Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 7:22-37 Biblia Habari Njema (BHN)

22. Basi, Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie Yohane yale mliyojionea na kuyasikia: Vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa Habari Njema.

23. Heri mtu yule ambaye hana mashaka nami!”

24. Hapo wajumbe wa Yohane walipokwisha kwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya watu juu ya Yohane: “Mlikwenda kutazama nini kule jangwani? Je, mlitaka kuona mwanzi unaotikiswa na upepo?

25. Basi, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona mtu aliyevaa mavazi maridadi? Wanaovaa mavazi maridadi na kuishi maisha ya anasa, hukaa katika majumba ya wafalme!

26. Basi, niambieni, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii.

27. Huyu Yohane ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu:‘Tazama mimi namtuma mtumishi wangu akutangulie;ambaye atakutayarishia njia yako.’”

28. Yesu akamalizia kwa kusema, “Nawaambieni, kati ya binadamu wote hakuna aliye mkubwa zaidi kuliko Yohane Mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika ufalme wa Mungu ni mkubwa kuliko yeye.”

29. Waliposikia hayo watu wote na watozaushuru waliusifu wema wa Mungu; hao ndio wale waliokuwa wameupokea ubatizo wa Yohane.

30. Lakini Mafarisayo na waalimu wa sheria walikataa mpango wa Mungu uliowahusu, wakakataa kubatizwa na Yohane.

31. Yesu akaendelea kusema, “Basi, nitawafananisha watu wa kizazi hiki na kitu gani? Ni watu wa namna gani?

32. Ni kama vijana waliokuwa wamekaa sokoni na kuambiana, kikundi kimoja na kingine:‘Tumewapigieni ngoma, lakini hamkucheza!Tumeimba nyimbo za huzuni lakini hamkulia!’

33. Kwa maana Yohane alikuja, akawa anafunga na hakunywa divai, nanyi mkasema: ‘Amepagawa na pepo!’

34. Naye Mwana wa Mtu amekuja, anakula na kunywa, nanyi mkasema: ‘Mwangalieni mlafi huyu na mlevi; rafiki ya watozaushuru na wenye dhambi!’

35. Hata hivyo, hekima ya Mungu imethibitishwa kuwa njema na wote wale wanaoikubali.”

36. Mfarisayo mmoja alimwalika Yesu kula chakula nyumbani kwake. Akaingia nyumbani kwa huyo Mfarisayo, akakaa kula chakula.

37. Basi, katika mji ule kulikuwa na mama mmoja mwenye dhambi. Alipopata habari kwamba Yesu yuko nyumbani kwa huyo Mfarisayo, alichukua chupa ya alabasta yenye marashi.

Kusoma sura kamili Luka 7