Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 7:2-13 Biblia Habari Njema (BHN)

2. Huko kulikuwa na jemadari mmoja ambaye alikuwa na mtumishi wake aliyempenda sana. Huyu mtumishi alikuwa mgonjwa karibu na kufa.

3. Yule jemadari aliposikia habari za Yesu, aliwatuma wazee fulani Wayahudi waende kumwomba aje kumponya mtumishi wake.

4. Walipofika kwa Yesu, walimsihi sana, wakasema: “Huyu anastahili afanyiwe jambo hilo,

5. kwa maana yeye analipenda taifa letu, na ndiye aliyetujengea lile sunagogi.”

6. Basi, Yesu akaenda pamoja nao. Alipokuwa karibu na kufika nyumbani kwa yule jemadari, yule jemadari aliwatuma marafiki zake wamwambie Yesu: “Bwana, usijisumbue zaidi, maana mimi sistahili uingie nyumbani mwangu.

7. Ndio maana sikujiona nastahili hata kuja kwako. Lakini sema tu neno, na mtumishi wangu atapona.

8. Kwa maana mimi pia ni mtu niliye chini ya mamlaka, na ninao askari chini yangu. Namwambia mmoja, ‘Nenda!’ Naye huenda; namwambia mwingine, ‘Njoo!’ Naye huja; na mtumishi wangu, ‘Fanya kitu hiki!’ Naye hufanya.”

9. Yesu aliposikia hayo, alishangaa, halafu akauelekea ule umati wa watu uliokuwa unamfuata, akasema, “Sijaona mwenye imani kama hii hata katika Israeli!”

10. Wale watu walipowasili nyumbani walimkuta yule mtumishi hajambo kabisa.

11. Baadaye kidogo, Yesu alikwenda katika mji mmoja uitwao Naini, na wafuasi wake na kundi kubwa la watu waliandamana naye.

12. Basi, alipokuwa anakaribia lango la mji, walitokea watu wamebeba maiti ya mwanamume mmoja, mtoto wa pekee wa mama mjane. Watu wengi wa mji ule walikuwa pamoja na huyo mama.

13. Bwana alipomwona mama huyo akamwonea huruma, akamwambia, “Usilie.”

Kusoma sura kamili Luka 7