Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 5:21-34 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Waalimu wa sheria na Mafarisayo wakaanza kujiuliza: “Nani huyu anayesema maneno ya kufuru? Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi ila Mungu peke yake!”

22. Yesu alitambua mawazo yao, akawauliza, “Mnawaza nini mioyoni mwenu?

23. Ni lipi lililo rahisi zaidi: Kusema, ‘Umesamehewa dhambi,’ au kusema, ‘Simama utembee?’

24. Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo wa kuwasamehe watu dhambi duniani.” Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Simama, chukua kitanda chako, uende zako nyumbani.”

25. Mara, huyo mtu aliyepooza akasimama mbele yao wote, akachukua kitanda chake akaenda nyumbani kwake huku akimtukuza Mungu.

26. Wote wakashangaa na kushikwa na hofu; wakamtukuza Mungu wakisema: “Tumeona maajabu leo.”

27. Baada ya hayo, Yesu akatoka nje, akamwona mtozaushuru mmoja aitwaye Lawi, ameketi ofisini. Yesu akamwambia, “Nifuate!”

28. Naye akaacha yote akamfuata.

29. Lawi akamwandalia Yesu karamu kubwa nyumbani mwake. Na kundi kubwa la watozaushuru na watu wengine walikuwa wameketi pamoja nao.

30. Mafarisayo na waalimu wa sheria wakawanungunikia wanafunzi wake wakisema: “Kwa nini mnakula na kunywa pamoja na watozaushuru na wenye dhambi?”

31. Yesu akawajibu, “Wenye afya hawamhitaji daktari; wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa.

32. Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi, wapate kutubu.”

33. Watu wengine wakamwambia, “Wafuasi wa Yohane Mbatizaji hufunga mara kwa mara na kusali; hata wafuasi wa Mafarisayo hufanya vivyo hivyo. Lakini wafuasi wako hula na kunywa.”

34. Yesu akawajibu, “Je, wale walioalikwa harusini hutakiwa wafunge hali bwana arusi yuko pamoja nao? La!

Kusoma sura kamili Luka 5