Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 3:3-19 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Basi, Yohane akaenda katika sehemu zote zilizopakana na mto Yordani. Akawa anahubiri watu watubu na kubatizwa ili Mungu awaondolee dhambi.

4. Ndivyo ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya:“Sauti ya mtu anaita jangwani:‘Mtayarishieni Bwana njia yake;nyosheni barabara zake.

5. Kila bonde litafukiwa,kila mlima na kilima vitasawazishwa;palipopindika patanyoshwa,njia mbaya zitatengenezwa.

6. Na, watu wote watauona wokovu aletao Mungu.’”

7. Basi, Yohane akawa anawaambia watu wengi waliofika ili awabatize: “Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea muikimbie ghadhabu inayokuja?

8. Onesheni kwa vitendo kwamba mmetubu. Msianze sasa kujisemea: ‘Baba yetu ni Abrahamu!’ Nawaambieni hakika, Mungu anaweza kuyafanya mawe haya yawe watoto wa Abrahamu.

9. Basi, shoka liko tayari kwenye mizizi ya miti; hivyo kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni.”

10. Umati wa watu ukamwuliza, “Tufanye nini basi?”

11. Akawajibu, “Aliye na nguo mbili amgawie yule asiye na nguo; aliye na chakula afanye vivyo hivyo.”

12. Nao watozaushuru wakaja pia ili wabatizwe, wakamwuliza, “Mwalimu, tufanye nini?”

13. Naye akawaambia, “Msitoze ushuru zaidi ya kima kilichowekwa.”

14. Nao askari wakamwuliza, “Na sisi tufanye nini?” Naye akawajibu, “Msichukue vitu vya mtu yeyote kwa nguvu wala kumshtaki yeyote kwa uongo. Toshekeni na mishahara yenu.”

15. Wote walikuwa wanatazamia kitu fulani; basi, wakaanza kujiuliza mioyoni mwao kuhusu Yohane, kuwa labda yeye ndiye Kristo.

16. Hapo Yohane akawaambia wote, “Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini anakuja mwenye uwezo kuliko mimi ambaye sistahili hata kumfungulia kamba za viatu vyake. Yeye atawabatizeni kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.

17. Yeye anacho mikononi mwake chombo cha kupuria nafaka aipure nafaka yake, akusanye ngano katika ghala, na makapi ayachome kwa moto usiozimika.”

18. Hivyo, pamoja na mawaidha mengine mengi, Yohane aliwahimiza watu akiwahubiria Habari Njema.

19. Lakini Yohane alimgombeza mtawala Herode, kwa sababu alikuwa amemchukua Herodia mke wa ndugu yake, na kumfanya mke wake; na pia kwa ajili ya mabaya yote aliyokuwa amefanya.

Kusoma sura kamili Luka 3