Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 3:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, Pontio Pilato alikuwa anatawala mkoa wa Yudea. Herode alikuwa mtawala wa Galilaya, na ndugu yake Filipo alikuwa mtawala wa eneo la Iturea na Trakoniti. Lusania alikuwa mtawala wa Abilene,

2. na Anasi na Kayafa walikuwa makuhani wakuu. Wakati huo ndipo neno la Mungu lilipomjia Yohane mwana wa Zakaria, kule jangwani.

3. Basi, Yohane akaenda katika sehemu zote zilizopakana na mto Yordani. Akawa anahubiri watu watubu na kubatizwa ili Mungu awaondolee dhambi.

4. Ndivyo ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya:“Sauti ya mtu anaita jangwani:‘Mtayarishieni Bwana njia yake;nyosheni barabara zake.

5. Kila bonde litafukiwa,kila mlima na kilima vitasawazishwa;palipopindika patanyoshwa,njia mbaya zitatengenezwa.

6. Na, watu wote watauona wokovu aletao Mungu.’”

7. Basi, Yohane akawa anawaambia watu wengi waliofika ili awabatize: “Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea muikimbie ghadhabu inayokuja?

8. Onesheni kwa vitendo kwamba mmetubu. Msianze sasa kujisemea: ‘Baba yetu ni Abrahamu!’ Nawaambieni hakika, Mungu anaweza kuyafanya mawe haya yawe watoto wa Abrahamu.

9. Basi, shoka liko tayari kwenye mizizi ya miti; hivyo kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni.”

10. Umati wa watu ukamwuliza, “Tufanye nini basi?”

11. Akawajibu, “Aliye na nguo mbili amgawie yule asiye na nguo; aliye na chakula afanye vivyo hivyo.”

Kusoma sura kamili Luka 3