Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 23:13-25 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Basi, Pilato akaitisha mkutano wa makuhani wakuu, viongozi na watu,

14. akawaambia, “Mmemleta mtu huyu kwangu mkisema kwamba alikuwa anawapotosha watu. Sasa sikilizeni! Baada ya kuchunguza jambo hilo mbele yenu, sikumpata na kosa lolote kuhusu mashtaka yenu juu yake.

15. Wala si mimi tu, bali hata Herode hakuona kosa lolote, kwa maana amemrudisha kwangu. Ni dhahiri kwamba mtu huyu hakufanya chochote kinachostahili adhabu ya kifo.

16. Hivyo, nitaamuru apigwe viboko, halafu nitamwachilia.” [

17. Kila sikukuu ya Pasaka, ilimlazimu Pilato kuwafungulia mfungwa mmoja.]

18. Lakini wote wakapiga kelele pamoja: “Mwondoe huyo, utufungulie Baraba!” (

19. Baraba alikuwa ametiwa ndani kwa kusababisha uasi katika mji na pia kwa sababu ya kuua.)

20. Pilato alitaka kumwachilia Yesu, hivyo akasema nao tena;

21. lakini wao wakapiga kelele: “Msulubishe, msulubishe!”

22. Pilato akawaambia mara ya tatu, “Amefanya ubaya gani? Sioni kosa lolote kwake linalomstahili auawe; kwa hiyo nitampiga viboko, halafu nimwachilie.”

23. Lakini wao wakazidi kupiga kelele kwa nguvu sana, kwamba Yesu ni lazima asulubiwe. Mwishowe, sauti zao zikashinda.

24. Basi, Pilato akaamua kwamba matakwa yao yatimizwe.

25. Akamfungua kutoka gerezani yule waliyemtaka, ambaye alikuwa ametiwa gerezani kwa kusababisha uasi na mauaji; akamtoa Yesu kwao, wamfanyie walivyotaka.

Kusoma sura kamili Luka 23