Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 2:8-20 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Katika sehemu hizo, walikuwako wachungaji wakikesha usiku mbugani kulinda mifugo yao.

9. Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukawaangazia pande zote. Wakaogopa sana.

10. Malaika akawaambia, “Msiogope! Nimewaleteeni habari njema ya furaha kubwa itakayowapata watu wote.

11. Kwa maana, leo hii katika mji wa Daudi, amezaliwa Mwokozi kwa ajili yenu, ndiye Kristo Bwana.

12. Na hiki kitakuwa kitambulisho kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelazwa horini.”

13. Mara kundi kubwa la jeshi la mbinguni likajiunga na huyo malaika, wakamsifu Mungu wakisema:

14. “Utukufu kwa Mungu juu mbinguni,na amani duniani kwa watu anaowafadhili!”

15. Baada ya hao malaika kuondoka na kurudi mbinguni, wachungaji wakaambiana: “Twendeni moja kwa moja mpaka Bethlehemu tukalione tukio hili Bwana alilotujulisha.”

16. Basi, wakaenda mbio, wakamkuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga amelazwa horini.

17. Hao wachungaji walipomwona mtoto huyo wakawajulisha wote habari waliyokuwa wamesikia juu yake.

18. Wote waliosikia hayo walishangaa juu ya habari walizoambiwa na wachungaji.

19. Lakini Maria aliyaweka na kuyatafakari mambo hayo yote moyoni mwake.

20. Wale wachungaji walirudi makwao huku wakimtukuza na kumsifu Mungu kwa yote waliyokuwa wamesikia na kuona; yote yalikuwa kama walivyokuwa wameambiwa.

Kusoma sura kamili Luka 2