Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 2:10-27 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Malaika akawaambia, “Msiogope! Nimewaleteeni habari njema ya furaha kubwa itakayowapata watu wote.

11. Kwa maana, leo hii katika mji wa Daudi, amezaliwa Mwokozi kwa ajili yenu, ndiye Kristo Bwana.

12. Na hiki kitakuwa kitambulisho kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelazwa horini.”

13. Mara kundi kubwa la jeshi la mbinguni likajiunga na huyo malaika, wakamsifu Mungu wakisema:

14. “Utukufu kwa Mungu juu mbinguni,na amani duniani kwa watu anaowafadhili!”

15. Baada ya hao malaika kuondoka na kurudi mbinguni, wachungaji wakaambiana: “Twendeni moja kwa moja mpaka Bethlehemu tukalione tukio hili Bwana alilotujulisha.”

16. Basi, wakaenda mbio, wakamkuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga amelazwa horini.

17. Hao wachungaji walipomwona mtoto huyo wakawajulisha wote habari waliyokuwa wamesikia juu yake.

18. Wote waliosikia hayo walishangaa juu ya habari walizoambiwa na wachungaji.

19. Lakini Maria aliyaweka na kuyatafakari mambo hayo yote moyoni mwake.

20. Wale wachungaji walirudi makwao huku wakimtukuza na kumsifu Mungu kwa yote waliyokuwa wamesikia na kuona; yote yalikuwa kama walivyokuwa wameambiwa.

21. Siku nane baadaye, wakati wa kumtahiri mtoto ulipofika, walimpa jina Yesu, jina ambalo alikuwa amepewa na malaika kabla hajachukuliwa mimba.

22. Siku zilipotimia za Yosefu na Maria kutakaswa kama walivyotakiwa na sheria, wazazi hao walimchukua mtoto, wakaenda naye Yerusalemu ili wamweke mbele za Bwana.

23. Katika sheria ya Bwana imeandikwa: “Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume atawekwa wakfu kwa Bwana.”

24. Pia walikwenda ili watoe sadaka: Hua wawili au makinda mawili ya njiwa, kama ilivyotakiwa katika sheria ya Bwana.

25. Wakati huo huko Yerusalemu kulikuwa na mtu mmoja, mwema na mcha Mungu, jina lake Simeoni. Yeye alikuwa akitazamia kwa hamu ukombozi wa Israeli. Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye.

26. Roho Mtakatifu alikuwa amemhakikishia kwamba hatakufa kabla ya kumwona Kristo wa Bwana.

27. Basi, akiongozwa na Roho Mtakatifu, Simeoni aliingia hekaluni; na wazazi wa Yesu walipomleta hekaluni mtoto wao ili wamfanyie kama ilivyotakiwa na sheria,

Kusoma sura kamili Luka 2