Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 18:14-25 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Nawaambieni, huyu mtozaushuru alirudi nyumbani akiwa amesamehewa. Lakini yule mwingine, sivyo. Kwa maana kila anayejikweza atashushwa, na kila anayejishusha atakwezwa.”

15. Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono yake. Wanafunzi walipowaona, wakawazuia kwa maneno makali.

16. Lakini Yesu akawaita kwake akisema: “Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu kama hawa.

17. Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hataingia katika ufalme huo.”

18. Kiongozi mmoja, Myahudi, alimwuliza Yesu, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niweze kuupata uhai wa milele?”

19. Yesu akamwambia, “Mbona waniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake.

20. Unazijua amri: ‘Usizini; Usiue; Usiibe; Usitoe ushahidi wa uongo; Waheshimu baba yako na mama yako.’”

21. Yeye akasema, “Hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu.”

22. Yesu aliposikia hayo, akamwambia, “Unatakiwa bado kufanya kitu kimoja: Uza kila kitu ulicho nacho, wagawie maskini hiyo fedha, nawe utakuwa na hazina yako mbinguni; halafu njoo unifuate.”

23. Lakini huyo mtu aliposikia hayo, alihuzunika sana kwa sababu alikuwa tajiri sana.

24. Yesu alipoona akihuzunika hivyo, akasema, “Jinsi gani ilivyo vigumu kwa matajiri kuingia katika ufalme wa Mungu!

25. Naam, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”

Kusoma sura kamili Luka 18