Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 17:21-37 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Wala hakuna atakayeweza kusema, ‘Uko hapa’, au ‘Uko pale’. Kwa kweli ufalme wa Mungu uko kati yenu.”

22. Halafu akawaambia wanafunzi wake, “Siku zinakuja ambapo mtatamani kuona mojawapo ya siku za Mwana wa Mtu, lakini hamtaiona.

23. Na watu watawaambieni: ‘Tazameni, yuko pale!’ Au ‘Tazameni, yupo hapa!’ Lakini nyinyi msitoke wala msiwafuate.

24. Kwa maana kama vile umeme unavyotokea ghafla na kuangaza anga upande mmoja hadi mwingine, ndivyo Mwana wa Mtu atakavyokuwa siku ile yake.

25. Lakini kabla ya hayo, itambidi ateseke sana na kukataliwa na kizazi hiki.

26. Kama ilivyokuwa nyakati za Noa, ndivyo itakavyokuwa katika siku za Mwana wa Mtu.

27. Watu waliendelea kula na kunywa, kuoa na kuolewa mpaka wakati ule Noa alipoingia katika safina. Gharika ikatokea na kuwaangamiza wote.

28. Itakuwa kama ilivyotokea wakati wa Loti. Watu waliendelea kula na kunywa, kununua na kuuza, kupanda mbegu na kujenga.

29. Lakini siku ile Loti alipoondoka Sodoma, moto na madini ya kiberiti vikanyesha kama mvua kutoka mbinguni na kuwaangamiza wote.

30. Ndivyo itakavyokuwa siku ile Mwana wa Mtu atakapofunuliwa.

31. “Siku hiyo, yeyote atakayekuwa juu ya paa asishuke kwenda nyumbani kuchukua mali yake. Kadhalika, naye atakayekuwa shambani asirudi nyuma.

32. Kumbukeni yaliyompata mke wa Loti.

33. Yeyote anayetaka kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na yeyote anayeipoteza, ataiokoa.

34. Nawaambieni, siku ile usiku watu wawili watakuwa wanalala pamoja, mmoja atachukuliwa na yule mwingine ataachwa.

35. Wanawake wawili watakuwa wakisaga nafaka pamoja; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.” [

36. Watu wawili watakuwa shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.]

37. Hapo wakamwuliza, “Ni wapi Bwana?” Naye akawaambia, “Palipo mzoga, ndipo tai watakapokusanyikia.”

Kusoma sura kamili Luka 17