Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 17:2-18 Biblia Habari Njema (BHN)

2. Ingekuwa afadhali kwake kufungiwa shingoni jiwe kubwa la kusagia na kutoswa baharini, kuliko kumkwaza mmoja wa wadogo hawa.

3. Jihadharini! Kama ndugu yako akikukosea, muonye; akitubu, msamehe.

4. Na kama akikukosea mara saba kwa siku, na kila mara akarudi kwako akisema, ‘Nimetubu,’ lazima umsamehe.”

5. Mitume wakamwambia Bwana, “Utuongezee imani.”

6. Naye Bwana akajibu, “Kama imani yenu ingekuwa ndogo hata kama chembe ndogo ya haradali, mngeweza kuuambia mti huu wa mkuyu: ‘Ngoka ukajipandikize baharini,’ nao ungewatii.

7. “Tuseme mmoja wenu ana mtumishi ambaye analima shambani au anachunga kondoo. Je, anaporudi kutoka shambani, atamwambia huyo mtumishi: ‘Haraka, njoo ule chakula?’

8. La! Atamwambia: ‘Nitayarishie chakula, ujifunge tayari kunitumikia mpaka nitakapomaliza kula na kunywa, ndipo nawe ule na kunywa.’

9. Je, utamshukuru huyo mtumishi kwa sababu ametimiza aliyoamriwa?

10. Hali kadhalika na nyinyi mkisha fanya yote mliyoamriwa, semeni: ‘Sisi ni watumishi tusio na faida, tumetimiza tu yale tuliyotakiwa kufanya.’”

11. Yesu akiwa safarini kwenda Yerusalemu alipitia katika mipaka ya Samaria na Galilaya.

12. Alipokuwa anaingia katika kijiji kimoja, watu kumi wenye ukoma walikutana naye, wakasimama kwa mbali.

13. Wakapaza sauti wakisema, “Yesu Mwalimu, tuonee huruma!”

14. Alipowaona akawaambia, “Nendeni mkajioneshe kwa makuhani.” Basi, ikawa walipokuwa wanakwenda, wakatakasika.

15. Mmoja wao alipoona kwamba ameponywa, alirudi akimtukuza Mungu kwa sauti kubwa.

16. Akajitupa chini mbele ya miguu ya Yesu huku akimshukuru. Huyo alikuwa Msamaria.

17. Hapo Yesu akasema, “Je, si watu kumi walitakaswa? Wale tisa wako wapi?

18. Hakupatikana mwingine aliyerudi kumtukuza Mungu ila tu huyu mgeni?”

Kusoma sura kamili Luka 17