Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 16:15-27 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Hapo akawaambia, “Nyinyi mnajifanya wema mbele ya watu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana kile kinachoonekana kuwa kitukufu mbele ya watu, Mungu anakiona kuwa takataka.

16. “Sheria na maandishi ya manabii vilikuwako mpaka wakati wa Yohane Mbatizaji. Tangu hapo, ufalme wa Mungu unahubiriwa, na kila mmoja anauingia kwa nguvu.

17. Lakini ni rahisi zaidi mbingu na dunia kupita, kuliko hata herufi moja ya sheria kufutwa.

18. “Yeyote anayempa mkewe talaka na kuoa mwingine, anazini; na yeyote anayemwoa mwanamke aliyepewa talaka, anazini.

19. “Palikuwa na mtu mmoja tajiri, ambaye alikuwa anavaa mavazi ya bei kubwa sana ya rangi ya zambarau na ya kitani safi, na kufanya sherehe kila siku.

20. Na, mlangoni pa huyo tajiri kulikuwa na maskini mmoja jina lake Lazaro, ambaye alikuwa amejaa vidonda.

21. Lazaro alitamani kupewa makombo yaliyoanguka kutoka mezani pa huyo tajiri; na zaidi ya hayo, mbwa walikuwa wanakuja na kuramba vidonda vyake!

22. “Basi, huyo maskini akafa, nao malaika wakamchukua, wakamweka karibu na Abrahamu. Na yule tajiri pia akafa, akazikwa.

23. Huyo tajiri, akiwa na mateso makali huko kuzimu, akainua macho yake, akamwona Abrahamu kwa mbali na Lazaro karibu naye.

24. Basi, akaita kwa sauti: ‘Babu Abrahamu, nionee huruma; umtume Lazaro angalau achovye ncha ya kidole chake katika maji, auburudishe ulimi wangu, maana ninateseka mno katika moto huu.’

25. Lakini Abrahamu akamjibu: ‘Kumbuka mwanangu kwamba ulipokea mema yako katika maisha, naye Lazaro akapokea mabaya. Sasa lakini, yeye anatulizwa, nawe unateswa.

26. Licha ya hayo, kati yetu na nyinyi kumewekwa shimo kubwa, ili wanaotaka kuja kwenu kutoka huku wasiweze, na wanaotaka kutoka kwenu kuja kwetu wasiweze.’

27. Huyo aliyekuwa tajiri akasema: ‘Basi babu, nakuomba umtume aende nyumbani kwa baba yangu,

Kusoma sura kamili Luka 16