Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 14:16-34 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alifanya karamu kubwa, akawaalika watu wengi.

17. Wakati wa karamu ulipofika alimtuma mtumishi wake akawaambie walioalikwa, ‘Njoni, kila kitu ni tayari.’

18. Lakini wote, mmoja baada ya mwingine, wakaanza kuomba radhi. Wa kwanza akamwambia mtumishi: ‘Nimenunua shamba, na hivyo sina budi niende kuliangalia; nakuomba uniwie radhi.’

19. Mwingine akasema: ‘Nimenunua ng'ombe jozi tano wa kulima, sasa nimo njiani kwenda kuwajaribu; nakuomba uniwie radhi.’

20. Na mwingine akasema: ‘Nimeoa kwa hiyo siwezi kuja.’

21. Mtumishi huyo akarudi na kumwarifu bwana wake jambo hilo. Yule mwenye nyumba alikasirika, akamwambia mtumishi wake: ‘Nenda upesi kwenye barabara na vichochoro vya mji, uwalete hapa ndani maskini, viwete, vipofu na vilema wengine.’

22. Baadaye, mtumishi huyo akasema: ‘Bwana, mambo yamefanyika kama ulivyoamuru, lakini bado iko nafasi.’

23. Yule bwana akamwambia mtumishi: ‘Nenda katika barabara na vichochoro vya mji uwashurutishe watu kuingia ili nyumba yangu ijae.

24. Kwa maana, nawaambieni, hakuna hata mmoja wa wale walioalikwa atakayeonja karamu yangu.’”

25. Hapo, makundi mengi yakawa yanaandamana pamoja na Yesu. Basi, akawageukia watu akawaambia,

26. “Mtu yeyote akija kwangu, asipomchukia baba yake, mama yake, mke wake, watoto, ndugu na dada zake, naam, hata na nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

27. Mtu asiyechukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

28. Kwa maana, ni nani miongoni mwenu ambaye akitaka kujenga mnara hataketi kwanza akadirie gharama zake ili ajue kama ana kiasi cha kutosha cha kumalizia?

29. La sivyo, baada ya kuweka msingi na kushindwa kumaliza, watu watamcheka

30. wakisema: ‘Mtu huyu alianza kujenga, lakini hakumalizia.’

31. “Au, ni mfalme gani ambaye akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, hataketi kwanza na kufikiri kama ataweza, kwa askari wake10,000, kumkabili yule aliye na askari 20,000?

32. Kama anaona hataweza, atawatuma wajumbe kutaka masharti ya amani wakati mfalme huyo mwingine angali mbali.

33. Vivyo hivyo, basi, hakuna hata mmoja wenu atakayekuwa mwanafunzi wangu kama asipoachilia kila kitu alicho nacho.

34. “Chumvi ni nzuri; lakini ikipoteza ladha yake, itakolezwa na nini?

Kusoma sura kamili Luka 14