Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 11:17-29 Biblia Habari Njema (BHN)

17. Lakini yeye, akiwa anayajua mawazo yao, akawaambia, “Ufalme wowote uliogawanyika vikundi vinavyopingana hauwezi kudumu; kadhalika, jamaa yoyote iliyo na mafarakano huangamia.

18. Kama Shetani anajipinga mwenyewe, utawala wake utasimamaje? Mnasemaje, basi, kwamba ninawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli?

19. Kama ninafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, wafuasi wenu huwafukuza kwa uwezo wa nani? Kwa sababu hiyo, wao ndio watakaowahukumu nyinyi.

20. Lakini ikiwa ninafukuza pepo kwa uwezo wa Mungu, basi jueni kwamba ufalme wa Mungu umekwisha fika kwenu.

21. “Mtu mwenye nguvu anapolinda jumba lake kwa silaha, mali yake yote iko salama.

22. Lakini akija mwenye nguvu zaidi akamshambulia na kumshinda, huyo huziteka silaha zake alizotegemea na kugawanya nyara.

23. Yeyote asiyejiunga nami, ananipinga; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya.

24. “Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu, huzururazurura jangwani kukavu akitafuta mahali pa kupumzika. Asipopata, hujisemea: ‘Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka.’

25. Anaporudi, huikuta ile nyumba imefagiwa na kupambwa.

26. Basi, huenda na kuwachukua pepo wengine saba wabaya kuliko yeye; wote huenda, wakamwingia mtu huyo. Hivyo, hali ya mtu huyo sasa huwa mbaya zaidi kuliko hapo mwanzo.”

27. Alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katika lile kundi la watu, akasema kwa sauti kubwa: “Heri mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyesha!”

28. Lakini Yesu akasema, “Lakini heri zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulishika.”

29. Umati wa watu ulipozidi kuongezeka, Yesu akawaambia, “Kizazi hiki ni kizazi kiovu. Kinataka ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ishara ya Yona.

Kusoma sura kamili Luka 11