Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 10:30-41 Biblia Habari Njema (BHN)

30. Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alikuwa anashuka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko. Alipokuwa njiani, alivamiwa na majambazi, wakamnyanganya mali yake na kumpiga, wakamwacha amelala pale nusu mfu.

31. Kumbe, kuhani mmoja akawa anapita barabara ileile, akamwona, akapita kando.

32. Hali kadhalika na Mlawi mmoja, alipofika mahali hapo akamwona, akapita kando.

33. Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa anasafiri, alifika pale yule mtu alipokuwa, naye alipomwona, alimwonea huruma.

34. Akamwendea, akamtibu majeraha yake kwa kumtia mafuta na divai na kuyafunga; halafu akampandisha juu ya punda wake, akampeleka katika nyumba moja ya wageni akamwuguza.

35. Kesho yake akatoa fedha dinari mbili akampa yule mwenye nyumba, akamwambia, ‘Mwuguze mtu huyu; na chochote utakachotumia zaidi, nitakulipa nitakaporudi.’”

36. Kisha Yesu akauliza, “Kati ya hao watatu, ni yupi aliyeonesha kuwa jirani yake yule aliyevamiwa na majambazi?”

37. Yule mwalimu wa sheria akamjibu, “Ni yule aliyemwonea huruma.” Yesu akamwambia, “Nenda ukafanye vivyo hivyo.”

38. Walipokuwa safarini, waliingia katika kijiji kimoja na mwanamke mmoja aitwaye Martha, akamkaribisha nyumbani kwake.

39. Martha alikuwa na dada yake aitwaye Maria; huyu aliketi karibu na Yesu akisikiliza mafundisho yake.

40. Lakini Martha alikuwa anashughulika na mambo mengi. Basi, akamwendea Yesu, akamwambia, “Bwana, hivi hujali kwamba dada yangu ameniacha nishughulike peke yangu? Mwambie basi, anisaidie.”

41. Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, unahangaika na kusumbuka kwa mambo mengi.

Kusoma sura kamili Luka 10