Agano la Kale

Agano Jipya

2 Petro 2:10-22 Biblia Habari Njema (BHN)

10. hasa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kupuuza mamlaka.Watu hao ni wakaidi na wenye majivuno, huvitukana na hawaviheshimu viumbe vitukufu vya juu.

11. Lakini malaika ambao wana uwezo na nguvu kuliko hao waalimu wa uongo, hawawashtaki na kuwatukana hao mbele ya Bwana.

12. Watu hao ambao hutukana chochote kile wasichoelewa, ni sawa na wanyama wasio na akili ambao huzaliwa na baadaye hukamatwa na kuchinjwa! Wataangamizwa kutokana na uharibifu wao wenyewe,

13. na watalipwa mateso kwa mateso ambayo wameyasababisha. Furaha yao ni kufanya, tena mchana kabisa, chochote kinachotosheleza anasa zao za mwili. Hao ni fedheha na aibu tupu kwa jumuiya yenu wakati wanapojiunga nanyi katika karamu zenu, hali wakifurahia njia zao za udanganyifu.

14. Macho yao yamejaa uzinzi na uwezo wao wa kutenda dhambi hauna kikomo. Huwaongoza watu walio dhaifu mpaka mitegoni. Mioyo yao imezoea kuwa na tamaa ya mali. Wapo chini ya laana ya Mungu!

15. Wameiacha njia iliyonyoka, wakapotoka na kuifuata njia aliyofuata Balaamu, mwana wa Beori ambaye alipendelea kupata faida kwa kufanya udanganyifu,

16. akakaripiwa kwa ajili ya uovu wake. Punda ambaye hasemi, alinena kwa sauti ya binadamu, akaukomesha wazimu wa huyo nabii.

17. Watu hao ni kama chemchemi zilizokauka, kama mawingu yanayopeperushwa na tufani; makao yao waliyowekewa ni mahali pa giza kuu.

18. Husema maneno ya majivuno na yasiyo na maana, na kutumia tamaa zao mbaya za kimwili kuwatega wale ambao wamejitenga hivi karibuni na watu waishio katika udanganyifu.

19. Huwaahidi watu wengine eti watakuwa huru, kumbe wao wenyewe ni watumwa wa upotovu – maana mtu ni mtumwa wa chochote kile kinachomtawala.

20. Watu waliokwisha ponyoka katika upotovu wa ulimwengu kwa kupata kumjua Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo, kisha wakakubali kunaswa na kutawaliwa tena na upotovu huo, hali yao itakuwa mbaya zaidi kuliko awali.

21. Ingalikuwa afadhali kwao kama wasingalijua kamwe njia hiyo ya uadilifu kuliko kuijua na kisha kuiacha na kupoteza amri takatifu waliyopokea.

22. Ipo methali isemayo: “Mbwa huyarudia matapishi yake mwenyewe,” na nyingine isemayo: “Nguruwe aliyekwisha oshwa hugaagaa tena katika matope!” Ndivyo ilivyo kwao sasa.

Kusoma sura kamili 2 Petro 2