Agano la Kale

Agano Jipya

1 Yohane 4:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Wapenzi wangu, msimsadiki kila mtu asemaye kwamba ana Roho wa Mungu, bali chunguzeni kwa makini kama huyo mtu anaongozwa na Roho wa Mungu au la, maana manabii wengi wa uongo wamezuka ulimwenguni.

2. Hii ndiyo njia ya kujua kama mtu anaongozwa na Roho wa Mungu: Kila anayekiri kwamba Kristo alikuja, akawa binadamu, mtu huyo anaye Roho wa Mungu.

3. Lakini mtu yeyote asiyemkiri Kristo hivyo, hana huyo Roho atokaye kwa Mungu. Mtu huyo ana roho ambaye ni wa mpinzani wa Kristo; nanyi mlikwisha sikia kwamba anakuja, na sasa tayari amekwisha wasili ulimwenguni!

4. Lakini nyinyi, watoto, ni wake Mungu na mmekwisha washinda hao manabii wa uongo; maana Roho aliye ndani yenu ana nguvu kuliko roho aliye ndani ya hao walio wa ulimwengu.

5. Wao husema mambo ya ulimwengu, nao ulimwengu huwasikiliza kwani wao ni wa ulimwengu.

6. Lakini sisi ni wake Mungu. Mtu anayemjua Mungu hutusikiliza, mtu asiye wa Mungu hatusikilizi. Basi, kwa njia hiyo tunaweza kutambua tofauti kati ya Roho wa ukweli na roho wa uongo.

7. Wapenzi wangu, tupendane, maana upendo hutoka kwa Mungu. Kila mtu aliye na upendo ni mtoto wa Mungu, na anamjua Mungu.

8. Mtu asiye na upendo hamjui Mungu, maana Mungu ni upendo.

9. Na Mungu alionesha upendo wake kwetu kwa kumtuma Mwanae wa pekee ulimwenguni, ili tuwe na uhai kwa njia yake.

10. Hivi ndivyo upendo ulivyo: Si kwamba sisi tulikuwa tumempenda Mungu kwanza, bali kwamba yeye alitupenda hata akamtuma Mwanae awe sadaka ya kutuondolea dhambi zetu.

11. Wapenzi wangu, ikiwa Mungu alitupenda hivyo, basi, nasi tunapaswa kupendana.

Kusoma sura kamili 1 Yohane 4