Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wakorintho 7:16-26 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Wewe mama Mkristo, unawezaje kuwa na hakika kwamba hutaweza kumwokoa mume wako? Au wewe mume Mkristo, unawezaje kuwa na hakika kwamba hutaweza kumwokoa mkeo?

17. Kwa vyovyote kila mmoja na aishi kufuatana na vipaji alivyogawiwa na Bwana, na kama alivyoitwa na Mungu. Hili ndilo agizo langu kwa makanisa yote.

18. Kama mtu aliitwa akiwa ametahiriwa, basi asijisingizie kwamba hakutahiriwa; na kama alipoitwa hakuwa ametahiriwa, basi na asitahiriwe.

19. Maana kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; kilicho muhimu ni kuzishika amri za Mungu.

20. Basi, kila mmoja na abaki kama alivyokuwa wakati alipoitwa.

21. Je, wewe ulikuwa mtumwa wakati ulipoitwa? Sawa, usijali; lakini ukipata fursa ya kuwa huru, itumie.

22. Maana yeye aliyeitwa na Bwana akiwa mtumwa huyo huwa mtu huru wa Bwana. Hali kadhalika naye aliyeitwa akiwa mtu huru, huwa mtumwa wa Kristo.

23. Nyote mmenunuliwa kwa bei; kwa hiyo msiwe tena watumwa wa watu.

24. Ndugu zangu, kila mmoja wenu basi, na abaki na Mungu kama alivyokuwa wakati alipoitwa.

25. Sasa, kuhusu mabikira na waseja, sina amri kutoka kwa Bwana; lakini natoa maoni yangu mimi ambaye kwa huruma yake Bwana nastahili kuaminiwa.

26. Basi, kutokana na shida iliyopo sasa nadhani ingefaa mtu abaki kama alivyo.

Kusoma sura kamili 1 Wakorintho 7