Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wakorintho 10:11-22 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Basi, mambo hayo yaliyowapata wao ni kielelezo kwa wengine, na yaliandikwa ili kutuonya sisi ambao mwisho wa nyakati unatukabili.

12. Anayedhani amesimama imara ajihadhari asianguke.

13. Majaribu mliyokwisha pata ni ya kawaida kwa binadamu. Mungu ni mwaminifu, naye hataruhusu mjaribiwe kupita nguvu zenu, ila pamoja na majaribu, yeye atawapeni pia nguvu ya kustahimili na njia ya kutoka humo salama.

14. Kwa hiyo, wapenzi wangu, epeni ibada za sanamu.

15. Naongea nanyi, watu wenye busara; jiamulieni wenyewe hayo nisemayo.

16. Tunapomshukuru Mungu kwa kikombe kile cha baraka, je, huwa hatushiriki damu ya Kristo? Na tunapoumega mkate, je, huwa hatushiriki mwili wa Kristo?

17. Kwa kuwa mkate huo ni mmoja, sisi, ingawa ni wengi, tu mwili mmoja; maana sote twashiriki mkate huohuo.

18. Angalieni kwa mfano Wayahudi wenyewe: Wale wanaokula tambiko wanaungana na hiyo madhabahu.

19. Nataka kusema nini, basi? Kwamba chakula kilichotambikiwa sanamu ni kitu zaidi ya chakula? Na hizo sanamu, je, ni kitu kweli zaidi ya sanamu?

20. Hata kidogo! Ninachosema ni kwamba tambiko wanazotoa watu wasiomjua Mungu wanawatolea pepo, sio Mungu. Sipendi kamwe nyinyi muwe na ushirika na pepo.

21. Hamwezi kunywa kikombe cha Bwana na kikombe cha pepo; hamwezi kushiriki katika Karamu ya Bwana na katika meza ya pepo.

22. Au je, tunataka kumfanya Bwana awe na wivu? Mnadhani tuna nguvu zaidi kuliko yeye?

Kusoma sura kamili 1 Wakorintho 10