1. Daudi alijijengea nyumba katika mji wa Daudi. Tena akalitengenezea sanduku la Mungu mahali, akalipigia hema.
2. Kisha akasema, “Hakuna mtu mwingine yeyote atakayelibeba sanduku la Mungu isipokuwa Walawi, maana Mwenyezi-Mungu aliwachagua wao kulibeba na kumtumikia milele.”
3. Basi, akawakusanya Waisraeli wote waje Yerusalemu, ili kulileta sanduku la Mwenyezi-Mungu mahali alipolitayarishia.
4. Halafu Daudi akawaita wazawa wa Aroni na Walawi:
5. Kutoka katika ukoo wa Kohathi, wakaja Urieli, pamoja na ndugu zake120 chini ya usimamizi wake;
6. kutoka katika ukoo wa Merari wakaja Asaya pamoja na ndugu zake 220 chini ya usimamizi wake;
7. kutoka katika ukoo wa Gershomu, wakaja Yoeli pamoja na ndugu zake 130 chini ya usimamizi wake;
8. kutoka katika ukoo ya Elisafani, wakaja Shemaya pamoja na ndugu zake 200 chini ya usimamizi wake;
9. kutoka katika ukoo wa Hebroni, wakaja Elieli pamoja na ndugu zake 80 chini ya usimamizi wake;
10. na kutoka katika ukoo wa Uzieli, wakaja Aminadabu pamoja na ndugu zake 112 chini ya usimamizi wake.
11. Daudi akawaita makuhani wawili: Sadoki na Abiathari, na Walawi sita: Urieli, Asaya, Yoeli, Shemaya, Elieli na Aminadabu;
12. akawaambia, “Nyinyi ni viongozi wa koo za Walawi. Jitakaseni pamoja na ndugu zenu, ili mkalilete sanduku la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, hadi mahali ambapo nimelitayarishia.
13. Kwa sababu hamkulibeba safari ya kwanza, Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alituadhibu kwani hatukulitunza kama alivyoagiza.”
14. Basi, makuhani na Walawi wakajitakasa ili wapate kulileta sanduku la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.
15. Walawi wakalibeba mabegani mwao wakitumia mipiko yake kama Mose alivyoamuru, kulingana na neno la Mwenyezi-Mungu.