Agano la Kale

Agano Jipya

Neh. 9:17-26 Swahili Union Version (SUV)

17. ila wakakataa kutii, wala hawakuyakumbuka maajabu yako, uliyoyafanya kati yao; lakini wakafanya shingo zao kuwa ngumu, na katika kuasi kwao wakaweka jemadari, ili wairudie hali ya utumwa; lakini wewe u Mungu, uliye tayari kusamehe, mwenye neema, mwenye huruma nyingi, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, basi hukuwaacha.

18. Naam, hata walipojifanyia ndama ya kusubu, na kusema, Huyu ndiye Mungu wako aliyekupandisha kutoka Misri, tena walipokuwa wamefanya machukizo makuu;

19. hata hivyo wewe kwa wingi wa rehema zako hukuwaacha jangwani; nguzo ya wingu haikuwaondokea wakati wa mchana, ili kuwaongoza njiani; wala nguzo ya moto haikuondoka wakati wa usiku, ili kuwapa mwanga na kuwaonyesha njia watakayoiendea.

20. Ukawapa na roho yako mwema ili kuwaelimisha, wala hukuwanyima mana vinywani mwao, tena ukawapa maji kwa ajili ya kiu yao.

21. Naam, muda wa miaka arobaini uliwaruzuku jangwani, wasihitaji kitu; nguo zao hazikuchakaa, wala miguu yao haikuvimba.

22. Pamoja na hayo ukawapa falme na taifa za watu, ulizowagawia sawasawa na mafungu yao; hivyo wakaimiliki nchi ya Sihoni, naam, nchi yake mfalme wa Heshboni, na nchi ya Ogu, mfalme wa Bashani.

23. Watoto wao nao uliwaongeza kama nyota za mbinguni, ukawaingiza katika nchi ile, uliyowaambia baba zao kuwa wataingia kuimiliki.

24. Basi wale watoto wakaingia wakaimiliki nchi, nawe ukawatiisha wenyeji wa nchi mbele yao, ndio Wakanaani, ukawatia mikononi mwao, pamoja na wafalme wao, na watu wa nchi, wawatende kama wapendavyo.

25. Wakaitwaa miji yenye boma, na nchi yenye neema, wakazitamalaki nyumba zilizojaa vitu vyema, birika zilizochimbwa, mizabibu, na mizeituni, na miti mingi yenye matunda; hivyo wakala, wakashiba, wakanenepa, wakajifurahisha katika wema wako mwingi.

26. Walakini hawakukutii, wakakuasi, wakaitupa sheria yako nyuma yao, wakawaua manabii wako walioshuhudu juu yao wapate kuwarejeza kwako; wakatenda machukizo makuu.

Kusoma sura kamili Neh. 9