Agano la Kale

Agano Jipya

Neh. 9:15-30 Swahili Union Version (SUV)

15. Ukawapa chakula toka mbinguni, kwa ajili ya njaa yao, na kwa ajili yao ukaleta maji kutoka mwambani, kwa sababu ya kiu yao, ukawaamuru kwamba waingie katika nchi na kuimiliki, ambayo umeinua mkono wako kuwapa.

16. Lakini wao na baba zetu wakatakabari, wakafanya shingo zao kuwa ngumu, wala hawakuzisikiliza amri zako,

17. ila wakakataa kutii, wala hawakuyakumbuka maajabu yako, uliyoyafanya kati yao; lakini wakafanya shingo zao kuwa ngumu, na katika kuasi kwao wakaweka jemadari, ili wairudie hali ya utumwa; lakini wewe u Mungu, uliye tayari kusamehe, mwenye neema, mwenye huruma nyingi, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, basi hukuwaacha.

18. Naam, hata walipojifanyia ndama ya kusubu, na kusema, Huyu ndiye Mungu wako aliyekupandisha kutoka Misri, tena walipokuwa wamefanya machukizo makuu;

19. hata hivyo wewe kwa wingi wa rehema zako hukuwaacha jangwani; nguzo ya wingu haikuwaondokea wakati wa mchana, ili kuwaongoza njiani; wala nguzo ya moto haikuondoka wakati wa usiku, ili kuwapa mwanga na kuwaonyesha njia watakayoiendea.

20. Ukawapa na roho yako mwema ili kuwaelimisha, wala hukuwanyima mana vinywani mwao, tena ukawapa maji kwa ajili ya kiu yao.

21. Naam, muda wa miaka arobaini uliwaruzuku jangwani, wasihitaji kitu; nguo zao hazikuchakaa, wala miguu yao haikuvimba.

22. Pamoja na hayo ukawapa falme na taifa za watu, ulizowagawia sawasawa na mafungu yao; hivyo wakaimiliki nchi ya Sihoni, naam, nchi yake mfalme wa Heshboni, na nchi ya Ogu, mfalme wa Bashani.

23. Watoto wao nao uliwaongeza kama nyota za mbinguni, ukawaingiza katika nchi ile, uliyowaambia baba zao kuwa wataingia kuimiliki.

24. Basi wale watoto wakaingia wakaimiliki nchi, nawe ukawatiisha wenyeji wa nchi mbele yao, ndio Wakanaani, ukawatia mikononi mwao, pamoja na wafalme wao, na watu wa nchi, wawatende kama wapendavyo.

25. Wakaitwaa miji yenye boma, na nchi yenye neema, wakazitamalaki nyumba zilizojaa vitu vyema, birika zilizochimbwa, mizabibu, na mizeituni, na miti mingi yenye matunda; hivyo wakala, wakashiba, wakanenepa, wakajifurahisha katika wema wako mwingi.

26. Walakini hawakukutii, wakakuasi, wakaitupa sheria yako nyuma yao, wakawaua manabii wako walioshuhudu juu yao wapate kuwarejeza kwako; wakatenda machukizo makuu.

27. Kwa sababu hiyo ukawatia katika mikono ya adui zao, waliowasumbua; na wakati wa shida yao, walipokulilia, uliwasikia kutoka mbinguni; na kwa wingi wa rehema zako ukawapa waokozi waliowaokoa katika mikono ya adui zao.

28. Lakini walipokuwa wamekwisha kustarehe, walitenda mabaya tena mbele zako; kwa hiyo ukawaacha katika mikono ya adui zao, nao wakawatawala; hata hivyo waliporejea na kukulilia, uliwasikia toka mbinguni; ukawaokoa mara nyingi kwa rehema zako;

29. ukawashuhudia ili uwarudishe tena katika sheria yako; lakini walitakabari, wasizisikilize amri zako, bali wakazihalifu hukumu zako, (ambazo mtu akizitenda ataishi katika hizo), nao wakayaondoa mabega yao, wakafanya shingo zao kuwa ngumu, wasitake kusikiliza.

30. Lakini miaka mingi ukachukuliana nao, nawe ukawashuhudia kwa roho yako kwa vinywa vya manabii wako; wao wasitake kusikiliza; kwa hiyo ukawatia katika mikono ya watu wa nchi.

Kusoma sura kamili Neh. 9