Sura

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12
  13. 13
  14. 14
  15. 15
  16. 16
  17. 17
  18. 18
  19. 19
  20. 20
  21. 21
  22. 22
  23. 23
  24. 24
  25. 25
  26. 26
  27. 27
  28. 28
  29. 29
  30. 30
  31. 31

Agano la Kale

Agano Jipya

Mit. 15 Swahili Union Version (SUV)

1. Jawabu la upole hugeuza hasira;Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.

2. Ulimi wa mwenye hekima hutamka maarifa vizuri;Bali vinywa vya wapumbavu humwaga upumbavu.

3. Macho ya BWANA yako kila mahali;Yakimchunguza mbaya na mwema.

4. Ulimi safi ni mti wa uzima;Bali ukorofi wa ulimi huvunja moyo.

5. Mpumbavu hudharau kurudiwa na babaye;Bali yeye aangaliaye maonyo hupata busara.

6. Katika nyumba ya mwenye haki mna akiba nyingi;Bali mapato ya mtu mbaya huwa taabu tu.

7. Midomo ya mwenye haki hueneza maarifa;Bali moyo wa mpumbavu haufanyi hivyo.

8. Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA;Bali maombi ya mtu mnyofu ni furaha yake.

9. Njia ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA;Bali humpenda mtu afuatiaye wema.

10. Adhabu kali ina yeye aiachaye njia;Naye achukiaye kukemewa atakufa.

11. Kuzimu na Uharibifu vi wazi mbele za BWANA;Si zaidi basi, mioyo ya wanadamu?

12. Mwenye mzaha hapendi kukaripiwa;Wala yeye hawaendei wenye hekima.

13. Moyo wa furaha huchangamsha uso;Bali kwa huzuni ya moyo roho hupondeka.

14. Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa;Bali kinywa cha wapumbavu hula upumbavu.

15. Siku zote za mtu ateswaye ni mbaya;Bali ukunjufu wa moyo ni karamu ya daima.

16. Kuwa na mali chache pamoja na kumcha BWANA;Ni bora kuliko mali nyingi pamoja na taabu.

17. Chakula cha mboga penye mapendano;Ni bora kuliko ng’ombe aliyenona pamoja na kuchukiana.

18. Mtu wa hasira huchochea ugomvi;Bali asiye mwepesi wa hasira hutuliza mashindano.

19. Njia ya mtu mvivu ni kama boma la miiba;Bali mapito yao wenye unyofu hufanyika njia kuu.

20. Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye;Bali mpumbavu humdharau mamaye.

21. Upumbavu ni furaha kwake aliyepungukiwa na akili;Bali mwenye ufahamu huunyosha mwenendo wake.

22. Pasipo mashauri makusudi hubatilika;Bali kwa wingi wa washauri huthibithika.

23. Mtu hulifurahia jibu la kinywa chake;Na neno linenwalo wakati wa kufaa ni jema kama nini!

24. Kwa mtu mwenye akili njia ya uhai huenda juu;Ili atoke katika kuzimu chini.

25. BWANA ataing’oa nyumba ya mwenye kiburi;Bali atauthibitisha mpaka wa mjane.

26. Mashauri mabaya ni chukizo kwa BWANA;Bali maneno yapendezayo ni safi.

27. Atamaniye faida huifadhaisha nyumba yake mwenyewe;Bali achukiaye zawadi ataishi.

28. Moyo wa mwenye haki hufikiri jinsi atakavyojibu;Bali kinywa cha wasio haki humwaga mabaya.

29. BWANA yu mbali na wasio haki;Bali huisikia sala ya mwenye haki.

30. Mng’ao wa macho huufurahisha moyo;Habari njema huinenepesha mifupa.

31. Sikio lisikilizalo lawama yenye uhaiLitakaa kati yao wenye hekima.

32. Akataaye maonyo huidharau nafsi yake mwenyewe;Bali yeye asikilizaye lawama hujipatia ufahamu.