Agano la Kale

Agano Jipya

Hos. 2:9-22 Swahili Union Version (SUV)

9. Basi kwa ajili ya hayo, nitaitwaa tena ngano yangu kwa wakati wake, na divai yangu kwa wakati wake, nami nitamnyang’anya sufu yangu na kitani yangu, vya kumfunika uchi wake.

10. Na sasa nitaifunua aibu yake mbele ya macho ya wapenzi wake, wala hapana mtu atakayemwokoa katika mkono wangu.

11. Tena nitaikomesha furaha yake yote, na sikukuu zake, na siku zake za mwandamo wa mwezi, na sabato zake, na makusanyiko yake yote yaliyoamriwa.

12. Nami nitaiharibu mizabibu yake na mitini yake, ambayo alisema, Hii ndiyo ujira wangu niliopewa na wapenzi wangu; nami nitaifanya kuwa msitu, na wanyama wa mashamba wataila.

13. Nami nitamwadhibu kwa sababu ya siku za Mabaali, aliowafukizia uvumba; hapo alipojipamba kwa pete masikioni mwake, na kwa vito asema BWANA.

14. Kwa hiyo angalia, mimi nitamshawishi, na kumleta nyikani, na kusema naye maneno ya kumtuliza moyo.

15. Nami nitampa mashamba yake ya mizabibu toka huko, na bonde la Akori kuwa mlango wa tumaini; naye ataniitikia huko, kama siku zile za ujana wake, na kama siku ile alipopanda kutoka nchi ya Misri.

16. Tena siku hiyo itakuwa, asema BWANA, utaniita Ishi, wala hutaniita tena Baali.

17. Kwa maana nitayaondoa majina ya Mabaali kinywani mwake, wala hawatatajwa tena kwa majina yao.

18. Nami siku hiyo nitafanya agano na wanyama wa mashamba kwa ajili yao, tena na ndege wa angani, tena na wadudu wa nchi; nami nitavivunja upinde na upanga na silaha vitoke katika nchi, nami nitawalalisha salama salimini.

19. Nami nitakuposa uwe wangu kwa milele; naam, nitakuposa kwa haki, na kwa hukumu, na kwa ufadhili, na kwa rehema.

20. Nami nitakuposa kwa uaminifu; nawe utamjua BWANA.

21. Tena itakuwa siku hiyo, mimi nitaitika, asema BWANA; nitaziitikia mbingu, nazo zitaiitikia nchi;

22. nayo nchi itaiitikia nafaka na divai na mafuta; nayo yataiitikia Yezreeli.

Kusoma sura kamili Hos. 2