Agano la Kale

Agano Jipya

Hos. 2:1-8 Swahili Union Version (SUV)

1. Waambieni ndugu zenu wanaume, Ami na ndugu zenu wanawake, Ruhama.

2. Msihini mama yenu, msihini; kwa maana yeye si mke wangu, wala mimi si mume wake; na ayawekee mbali mambo ya uasherati wake yasiwe mbele ya uso wake, na mambo ya uzinzi wake yasiwe kati ya maziwa yake;

3. nisije nikamvua nguo zake akawa uchi, nikamweka katika hali aliyokuwa nayo siku ya kuzaliwa kwake, na kumfanya kama jangwa, na kumweka kama nchi kame, na kumfisha kwa kiu;

4. naam, sitawaonea rehema watoto wake; kwa maana ni watoto wa uzinzi.

5. Maana mama yao amezini; yeye aliyewachukua mimba ametenda mambo ya aibu; maana alisema, Nitafuatana na wapenzi wangu, wanipao chakula changu na maji yangu, sufu yangu na kitani yangu, mafuta yangu na vileo vyangu.

6. Basi kwa ajili ya hayo, angalia, nitaiziba njia yako kwa miiba, nami nitafanya kitalu juu yake, asipate kuyaona mapito yake.

7. Naye atawafuata wapenzi wake, lakini hatawapata; atawatafuta, lakini hatawaona; ndipo atakaposema, Nitakwenda nikamrudie mume wangu wa kwanza; kwa maana hali yangu ya zamani ilikuwa njema kuliko hali yangu ya sasa.

8. Maana hakujua ya kuwa mimi ndiye aliyempa ngano, na divai, na mafuta, na kumwongezea fedha na dhahabu, walivyovitumia kwa ajili ya Baali.

Kusoma sura kamili Hos. 2