Agano la Kale

Agano Jipya

Yud. 1:10-20 Swahili Union Version (SUV)

10. Lakini watu hawa huyatukana mambo wasiyoyajua, na mambo wayatambuayo kwa asili wajiharibu kwayo kama wanyama wasio na akili.

11. Ole wao! Kwa sababu walikwenda katika njia ya Kaini, na kulifuata kosa la Balaamu pasipo kujizuia, kwa ajili ya ujira, nao wameangamia katika maasi ya Kora.

12. Watu hawa ni miamba yenye hatari katika karamu zenu za upendo walapo karamu pamoja nanyi, wakijilisha pasipo hofu; ni mawingu yasiyo na maji, yachukuliwayo na upepo; ni miti iliyopukutika, isiyo na matunda, iliyokufa mara mbili, na kung’olewa kabisa;

13. ni mawimbi ya bahari yasiyozuilika, yakitoa aibu yao wenyewe kama povu; ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba yao waliowekewa milele.

14. Na Henoko, mtu wa saba baada ya Adamu, alitoa maneno ya unabii juu ya hao, akisema, Angalia, Bwana alikuja na watakatifu wake, maelfu maelfu,

15. ili afanye hukumu juu ya watu wote, na kuwaadhibisha wote wasiomcha Mungu, kwa ajili ya kazi zao zote za upotevu walizozitenda bila kumcha Mungu, na kwa ajili ya maneno magumu yote ambayo hao wenye dhambi wasiomcha Mungu wameyanena juu yake.

16. Watu hawa ni wenye kunung’unika, wenye kulalamika, waendao kwa tamaa zao, na vinywa vyao vyanena maneno makuu mno ya kiburi, wakipendelea watu wenye cheo kwa ajili ya faida.

17. Bali ninyi, wapenzi, yakumbukeni maneno yaliyonenwa zamani na mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo,

18. ya kwamba waliwaambia ya kuwa, Wakati wa mwisho watakuwako watu wenye kudhihaki, wakizifuata tamaa zao wenyewe za upotevu.

19. Watu hao ndio waletao matengano, watu wa dunia hii tu, wasio na Roho.

20. Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu,

Kusoma sura kamili Yud. 1