Agano la Kale

Agano Jipya

Yn. 9:2-15 Swahili Union Version (SUV)

2. Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu?

3. Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake.

4. Imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenipeleka maadamu ni mchana, usiku waja asipoweza mtu kufanya kazi.

5. Muda nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.

6. Alipokwisha kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu tope za macho,

7. akamwambia, Nenda kanawe katika birika ya Siloamu, (maana yake, Aliyetumwa). Basi akaenda na kunawa; akarudi anaona.

8. Basi jirani zake, na wale waliomwona zamani kuwa ni mwombaji, wakasema, Je! Huyu siye yule aliyekuwa akiketi na kuomba?

9. Wengine wakasema, Ndiye. Wengine wakasema, La, lakini amefanana naye. Yeye mwenyewe alisema, Mimi ndiye.

10. Basi wakamwambia, Macho yako yalifumbuliwaje?

11. Yeye akajibu, Mtu yule aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka macho akaniambia, Nenda Siloamu ukanawe; basi nikaenda na kunawa, nikapata kuona.

12. Wakamwambia, Yuko wapi huyo? Akasema, Mimi sijui.

13. Basi wakampeleka kwa Mafarisayo yule aliyekuwa kipofu zamani.

14. Nayo ilikuwa sabato, hapo Yesu alipofanya zile tope na kumfumbua macho.

15. Basi Mafarisayo nao wakamwuliza tena jinsi gani alivyopata kuona. Akawaambia, Alinitia tope juu ya macho, nami nikanawa, na sasa naona.

Kusoma sura kamili Yn. 9