Agano la Kale

Agano Jipya

Yn. 7:11-26 Swahili Union Version (SUV)

11. Basi Wayahudi wakamtafuta kwenye sikukuu, wakasema, Yuko wapi yule?

12. Kukawa na manung’uniko mengi katika makutano juu yake. Wengine wakasema, Ni mtu mwema. Na wengine wakasema, Sivyo; bali anawadanganya makutano.

13. Walakini hakuna mtu aliyemtaja waziwazi, kwa sababu ya kuwaogopa Wayahudi.

14. Hata ikawa katikati ya sikukuu Yesu alikwea kuingia hekaluni, akafundisha.

15. Wayahudi wakastaajabu wakisema, Amepataje huyu kujua elimu, ambaye hakusoma?

16. Basi Yesu akawajibu, akasema, Mafunzo yangu si yangu mimi, ila ni yake yeye aliyenipeleka.

17. Mtu akipenda kuyatenda mapenzi yake, atajua habari ya yale mafunzo, kwamba yatoka kwa Mungu, au kwamba mimi nanena kwa nafsi yangu tu.

18. Yeye anenaye kwa nafsi yake tu hutafuta utukufu wake mwenyewe; bali yeye anayetafuta utukufu wake aliyempeleka, huyo ni wa kweli, wala ndani yake hamna udhalimu.

19. Je! Musa hakuwapa torati? Wala hakuna mmoja wenu aitendaye torati. Mbona mnatafuta kuniua?

20. Mkutano wakajibu, Ama! Una pepo! Ni nani anayetafuta kukuua?

21. Yesu akajibu, akawaambia, Mimi nalitenda kazi moja, nanyi nyote mnaistaajabia.

22. Musa aliwapa tohara; lakini si kwamba yatoka kwa Musa, bali kwa mababa; nanyi siku ya sabato humtahiri mtu.

23. Basi ikiwa mtu hupashwa tohara siku ya sabato, ili torati ya Musa isije ikavunjika, mbona mnanikasirikia mimi kwa sababu nalimfanya mtu kuwa mzima kabisa siku ya sabato?

24. Basi msihukumu hukumu ya macho tu, bali ifanyeni hukumu iliyo ya haki.

25. Basi baadhi ya watu wa Yerusalemu wakasema, Je! Huyu siye wanayemtafuta ili wamwue?

26. Na kumbe! Anena waziwazi, wala hawamwambii neno! Yamkini hao wakuu wanajua hakika ya kuwa huyu ndiye Kristo?

Kusoma sura kamili Yn. 7