Agano la Kale

Agano Jipya

Yn. 7:1-16 Swahili Union Version (SUV)

1. Na baada ya hayo Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya; maana hakutaka kutembea katika Uyahudi, kwa sababu Wayahudi walikuwa wakitafuta kumwua.

2. Na sikukuu ya Wayahudi, Sikukuu ya Vibanda, ilikuwa karibu.

3. Basi ndugu zake wakamwambia, Ondoka hapa, uende Uyahudi, wanafunzi wako nao wapate kuzitazama kazi zako unazozifanya.

4. Kwa maana hakuna mtu afanyaye neno kwa siri, naye mwenyewe ataka kujulikana. Ukifanya mambo haya, basi jidhihirishe kwa ulimwengu.

5. Maana hata nduguze hawakumwamini.

6. Basi Yesu akawaambia, Haujafika bado wakati wangu; ila wakati wenu sikuzote upo.

7. Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi; bali hunichukia mimi, kwa sababu mimi naushuhudia ya kuwa kazi zake ni mbovu.

8. Kweeni ninyi kwenda kula sikukuu; mimi sikwei bado kwenda kula sikukuu hii, kwa kuwa haujatimia wakati wangu.

9. Naye alipokwisha kuwaambia hayo, alikaa vivi hivi huko Galilaya.

10. Hata ndugu zake walipokwisha kukwea kuiendea sikukuu, ndipo yeye naye alipokwea, si kwa wazi bali kana kwamba kwa siri.

11. Basi Wayahudi wakamtafuta kwenye sikukuu, wakasema, Yuko wapi yule?

12. Kukawa na manung’uniko mengi katika makutano juu yake. Wengine wakasema, Ni mtu mwema. Na wengine wakasema, Sivyo; bali anawadanganya makutano.

13. Walakini hakuna mtu aliyemtaja waziwazi, kwa sababu ya kuwaogopa Wayahudi.

14. Hata ikawa katikati ya sikukuu Yesu alikwea kuingia hekaluni, akafundisha.

15. Wayahudi wakastaajabu wakisema, Amepataje huyu kujua elimu, ambaye hakusoma?

16. Basi Yesu akawajibu, akasema, Mafunzo yangu si yangu mimi, ila ni yake yeye aliyenipeleka.

Kusoma sura kamili Yn. 7