Agano la Kale

Agano Jipya

Yn. 4:21-35 Swahili Union Version (SUV)

21. Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu.

22. Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi.

23. Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.

24. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.

25. Yule mwanamke akamwambia, Najua ya kuwa yuaja Masihi, (aitwaye Kristo); naye atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote.

26. Yesu akamwambia, Mimi ninayesema nawe, ndiye.

27. Mara hiyo wakaja wanafunzi wake, wakastaajabu kwa sababu alikuwa akisema na mwanamke; lakini hakuna aliyesema, Unatafuta nini? Au, Mbona unasema naye?

28. Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini, akawaambia watu,

29. Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo?

30. Basi wakatoka mjini, wakamwendea.

31. Huko nyuma wanafunzi wakamsihi wakisema, Rabi, ule.

32. Akawaambia, Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi.

33. Basi wanafunzi wake wakasemezana, Je! Mtu amemletea chakula?

34. Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake.

35. Hamsemi ninyi, Bado miezi minne, ndipo yaja mavuno? Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno.

Kusoma sura kamili Yn. 4