Agano la Kale

Agano Jipya

Yn. 2:1-16 Swahili Union Version (SUV)

1. Na siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo.

2. Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake.

3. Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, Hawana divai.

4. Yesu akamwambia, Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia.

5. Mamaye akawaambia watumishi, Lo lote atakalowaambia, fanyeni.

6. Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu.

7. Yesu akawaambia, Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza hata juu.

8. Akawaambia, Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza. Wakapeleka.

9. Naye mkuu wa meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, (wala asijue ilikotoka, lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maji), yule mkuu wa meza alimwita bwana arusi,

10. akamwambia, Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa.

11. Mwanzo huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.

12. Baada ya hayo akashuka mpaka Kapernaumu, yeye na mama yake na ndugu zake na wanafunzi wake; wakakaa huko siku si nyingi.

13. Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; naye Yesu akakwea mpaka Yerusalemu.

14. Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng’ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi.

15. Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng’ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao;

16. akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara.

Kusoma sura kamili Yn. 2