Agano la Kale

Agano Jipya

Yn. 18:1-15 Swahili Union Version (SUV)

1. Alipokwisha kusema hayo, Yesu alitoka pamoja na wanafunzi wake kwenda ng’ambo ya kijito Kedroni, palipokuwapo bustani; akaingia yeye na wanafunzi wake.

2. Naye Yuda, yule aliyetaka kumsaliti, alipajua mahali pale; kwa sababu Yesu alikuwa akienda huko mara nyingi pamoja na wanafunzi wake.

3. Basi Yuda, akiisha kupokea kikosi cha askari na watumishi waliotoka kwa wakuu wa makuhani na Mafarisayo, akaenda huko na taa na mienge na silaha.

4. Basi Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawaambia, Ni nani mnayemtafuta?

5. Wao wakamjibu, Ni Yesu Mnazareti. Yesu akawaambia, Ni mimi. Yuda naye aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao.

6. Basi alipowaambia, Ni mimi, walirudi nyuma, wakaanguka chini.

7. Basi akawauliza tena, Mnamtafuta nani? Wakasema, Yesu Mnazareti.

8. Yesu akajibu, Nimekwisha kuwaambieni ya kwamba ni mimi; basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao.

9. Ili litimizwe lile neno alilolisema, Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja wao.

10. Basi Simoni Petro alikuwa na upanga, akaufuta, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume. Na yule mtumwa jina lake ni Malko.

11. Basi Yesu akamwambia Petro, Rudisha upanga alani mwake; je! Kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee?

12. Basi wale askari na yule jemadari na wale watumishi wa Wayahudi walimkamata Yesu, wakamfunga.

13. Wakamchukua kwa Anasi kwanza; maana alikuwa mkwewe Kayafa, yule aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule.

14. Naye Kayafa ndiye yule aliyewapa Wayahudi lile shauri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu.

15. Wakamfuata Yesu, Petro na mwanafunzi mwingine. Na mwanafunzi huyo alikuwa amejulikana na Kuhani Mkuu, akaingia pamoja na Yesu katika behewa ya Kuhani Mkuu.

Kusoma sura kamili Yn. 18