1. Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi.
2. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali.
3. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.
4. Nami niendako mwaijua njia.
5. Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia?
6. Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
7. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona.
8. Filipo akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha.
9. Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?