Agano la Kale

Agano Jipya

Yn. 12:39-50 Swahili Union Version (SUV)

39. Ndiyo sababu wao hawakuweza kusadiki; kwa maana Isaya alisema tena,

40. Amewapofusha macho,Ameifanya mizito mioyo yao;Wasije wakaona kwa macho yao,Wakafahamu kwa mioyo yao,Wakaongoka, nikawaponya.

41. Maneno hayo aliyasema Isaya, kwa kuwa aliuona utukufu wake, akataja habari zake.

42. Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi.

43. Kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu.

44. Naye Yesu akapaza sauti, akasema, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye aliyenipeleka.

45. Naye anitazamaye mimi amtazama yeye aliyenipeleka.

46. Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani.

47. Na mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu.

48. Yeye anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye; neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho.

49. Kwa sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu; bali Baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema.

50. Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi, kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo.

Kusoma sura kamili Yn. 12