Agano la Kale

Agano Jipya

Yn. 10:10-21 Swahili Union Version (SUV)

10. Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.

11. Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.

12. Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya.

13. Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake.

14. Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi;

15. kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo.

16. Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.

17. Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena.

18. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu.

19. Kukaingia tena matengano kati ya Wayahudi, kwa ajili ya maneno hayo.

20. Wengi wao wakasema, Ana pepo huyu, tena ana wazimu; mbona mnamsikiliza?

21. Wengine wakasema, Maneno hayo siyo ya mtu mwenye pepo. Je! Pepo aweza kuwafumbua macho vipofu?

Kusoma sura kamili Yn. 10