Agano la Kale

Agano Jipya

Ufu. 17:3-13 Swahili Union Version (SUV)

3. Akanichukua katika Roho hata jangwani, nikaona mwanamke, ameketi juu ya mnyama mwekundu sana, mwenye kujaa majina ya makufuru, mwenye vichwa saba na pembe kumi.

4. Na mwanamke yule alikuwa amevikwa nguo ya rangi ya zambarau, na nyekundu, amepambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu, naye alikuwa na kikombe cha dhahabu mkononi mwake, kilichojawa na machukizo, na machafu ya uasherati wake.

5. Na katika kipaji cha uso wake alikuwa na jina limeandikwa, la siri, BABELI MKUU, MAMA WA MAKAHABA NA MACHUKIZO YA NCHI.

6. Nikamwona yule mwanamke amelewa kwa damu ya watakatifu, na kwa damu ya mashahidi wa Yesu. Nami nilipomwona nikastaajabu ajabu kuu.

7. Na yule malaika akaniambia, Kwani kustaajabu? Nitakuambia siri ya mwanamke huyu, na ya mnyama huyu amchukuaye, mwenye vile vichwa saba na zile pembe kumi.

8. Yule mnyama uliyemwona alikuwako, naye hayuko, naye yu tayari kupanda kutoka kuzimu na kwenda kwenye uharibifu. Na hao wakaao juu ya nchi, wasioandikwa majina yao katika kitabu cha uzima tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu, watastaajabu wamwonapo yule mnyama, ya kwamba alikuwako, naye hayuko, naye atakuwako.

9. Hapo ndipo penye akili zenye hekima. Vile vichwa saba ni milima saba anayokalia mwanamke huyo.

10. Navyo ni wafalme saba. Watano wamekwisha kuanguka, na mmoja yupo, na mwingine hajaja bado. Naye atakapokuja imempasa kukaa muda mchache.

11. Na yule mnyama aliyekuwako naye hayuko, yeye ndiye wa nane, naye ni mmoja wa wale saba, naye aenenda kwenye uharibifu.

12. Na zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme kumi, ambao hawajapokea ufalme bado, lakini wapokea mamlaka kama wafalme muda wa saa moja pamoja na yule mnyama.

13. Hawa wana shauri moja, nao wampa yule mnyama nguvu zao na mamlaka yao.

Kusoma sura kamili Ufu. 17