Agano la Kale

Agano Jipya

Ufu. 11:1-14 Swahili Union Version (SUV)

1. Nikapewa mwanzi kama fimbo; na mmoja akaniambia, Inuka, ukalipime hekalu la Mungu, na madhabahu, na hao wasujuduo humo.

2. Na behewa iliyo nje ya hekalu uiache nje wala usiipime, kwa maana Mataifa wamepewa hiyo, nao wataukanyaga mji mtakatifu miezi arobaini na miwili.

3. Nami nitawaruhusu mashahidi wangu wawili, nao watatoa unabii siku elfu na mia mbili na sitini, hali wamevikwa magunia.

4. Hao ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili visimamavyo mbele za Bwana wa nchi.

5. Na mtu akitaka kuwadhuru, moto hutoka katika vinywa vyao na kuwala adui zao. Na mtu akitaka kuwadhuru, hivyo ndivyo impasavyo kuuawa.

6. Hao wana amri ya kuzifunga mbingu, ili mvua isinyeshe katika siku za unabii wao. Nao wana amri juu ya maji kuyageuza kuwa damu, na kuipiga nchi kwa kila pigo, kila watakapo.

7. Hata watakapoumaliza ushuhuda wao, yule mnyama atokaye katika kuzimu atafanya vita nao, naye atawashinda na kuwaua.

8. Na mizoga yao itakuwa katika njia ya mji ule mkuu, uitwao kwa jinsi ya roho Sodoma, na Misri, tena ni hapo Bwana wao aliposulibiwa.

9. Na watu wa hao jamaa na kabila na lugha na taifa waitazama mizoga yao siku tatu u nusu, wala hawaiachi mizoga yao kuwekwa kaburini.

10. Nao wakaao juu ya nchi wafurahi juu yao na kushangilia. Nao watapelekeana zawadi wao kwa wao, kwa kuwa manabii hao wawili waliwatesa wao wakaao juu ya nchi.

11. Na baada ya siku hizo tatu u nusu, roho ya uhai itokayo kwa Mungu ikawaingia, wakasimama juu ya miguu yao; na hofu kuu ikawaangukia watu waliowatazama.

12. Wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, Pandeni hata huku. Wakapanda mbinguni katika wingu, adui zao wakiwatazama.

13. Na katika saa ile palikuwa na tetemeko kuu la nchi, na sehemu ya kumi ya mji ikaanguka; wanadamu elfu saba wakauawa katika tetemeko lile. Na waliosalia wakaingiwa na hofu, wakamtukuza Mungu wa mbingu.

14. Ole wa pili umekwisha pita, tazama ole wa tatu unakuja upesi.

Kusoma sura kamili Ufu. 11