Agano la Kale

Agano Jipya

Mdo 27:6-21 Swahili Union Version (SUV)

6. Na huko yule akida akakuta merikebu ya Iskanderia, tayari kusafiri kwenda Italia, akatupandisha humo.

7. Tukasafiri polepole kwa muda wa siku nyingi, tukafika mpaka Nido kwa shida; na kwa sababu upepo ulikuwa ukituzuia tukapita chini ya Krete, tukaikabili Salmone.

8. Tukaipita kwa shida, pwani kwa pwani, tukafika mahali paitwapo Bandari Nzuri. Karibu na hapo pana mji uitwao Lasea.

9. Na wakati mwingi ulipokwisha kupita, na safari ikiwa ina hatari sasa, kwa sababu siku za kufunga zilikuwa zimekwisha kupita, Paulo akawaonya,

10. akawaambia, Wanaume, naona kwamba safari hii itakuwa na madhara na hasara nyingi, si ya shehena na merikebu tu, ila na ya maisha yetu pia.

11. Lakini yule akida akawasikiliza nahodha na mwenye merikebu zaidi ya yale aliyoyasema Paulo.

12. Na kwa sababu bandari ile ilikuwa haifai kukaa wakati wa baridi, wengi wao wakatoa shauri la kutweka kutoka huko ili wapate kufika Foinike, kama ikiwezekana, na kukaa huko wakati wa baridi; nayo ni bandari ya Krete, inaelekea kaskazini-mashariki na kusini-mashariki.

13. Na upepo wa kusi ulipoanza kuvuma kidogo, wakidhani ya kuwa wamepata waliyoazimu kupata, wakang’oa nanga, wakasafiri karibu na Krete pwani kwa pwani.

14. Baada ya muda mchache ukavuma upepo wa nguvu wa namna ya tufani, uitwao Eurakilo,

15. merikebu iliposhikwa, na kutoweza kushindana na upepo, tukaiacha tukachukuliwa.

16. Na tukipita upesi karibu na kisiwa kidogo kiitwacho Kauda tukadiriki kuikweza mashua; lakini kwa shida.

17. Walipokwisha kuikweza wakatumia misaada, wakaikaza merikebu kwa kupitisha kamba chini yake, nao wakiogopa wasije wakakwama katika fungu liitwalo Sirti, wakatua matanga wakachukuliwa vivi hivi.

18. Na kwa maana tulikuwa tukipigwa sana na ile tufani, siku ya pili yake wakaanza kuitupa shehena baharini.

19. Siku ya tatu wakatupa vyombo vya merikebu kwa mikono yao wenyewe.

20. Jua wala nyota hazikuonekana kwa muda wa siku nyingi, na tufani kuu ikatushika, basi tukakata tamaa ya kuokoka.

21. Na walipokuwa wamekaa wakati mwingi bila kula chakula, Paulo akasimama katikati yao, akasema, Wanaume, iliwapasa kunisikiliza mimi na kutokung’oa nanga huko Krete, na kupata madhara haya na hasara hii.

Kusoma sura kamili Mdo 27