Agano la Kale

Agano Jipya

Mdo 27:31-44 Swahili Union Version (SUV)

31. Paulo akawaambia akida na askari, Hawa wasipokaa ndani ya merikebu hamtaweza kuokoka.

32. Basi askari wakazikata kamba za mashua, wakaiacha ianguke.

33. Na kulipokuwa kukipambauka Paulo akawasihi wote wale chakula, akisema, Leo ni siku ya kumi na nne kungoja na kufunga, hamkula kitu cho chote.

34. Basi nawasihi mle chakula, maana itakuwa kwa wokovu wenu; kwa maana hapana hata unywele wa kichwa cha mmoja wenu utakaopotea.

35. Alipokwisha kusema hayo akatwaa mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote akaumega akaanza kula.

36. Ndipo wakachangamka wote, wakala chakula wenyewe.

37. Na sisi tuliokuwa ndani ya merikebu tulipata watu mia mbili na sabini na sita.

38. Walipokwisha kushiba wakaipunguza shehena ya merikebu, wakiitupa ngano baharini.

39. Kulipokucha hawakuitambua ile nchi, ila waliona hori yenye ufuo, wakashauriana kuiegesha merikebu huko, kama ikiwezekana.

40. Wakazitupilia mbali zile nanga, na kuziacha baharini, pamoja na kuzilegeza kamba za sukani, wakalitweka tanga dogo ili liushike upepo, wakauendea ule ufuo.

41. Lakini wakafikia mahali palipokutana bahari mbili, wakaiegesha merikebu, omo ikakwama ikakaa isitikiswe, bali tezi ilikuwa imefumuliwa kwa nguvu za mawimbi.

42. Shauri la askari lilikuwa kuwaua wafungwa, mtu asiogelee na kukimbia.

43. Bali akida, akitaka kumponya Paulo, akawazuia, wasifanye kama walivyokusudia, akawaamuru wale wawezao kuogelea wajitupe kwanza baharini, wafike nchi kavu;

44. nao waliosalia, hawa juu ya mbao na hawa juu ya vitu vingine vya merikebu. Na hivyo watu wote wakapata kuifikilia nchi kavu salama.

Kusoma sura kamili Mdo 27