Agano la Kale

Agano Jipya

Ebr. 11:19-39 Swahili Union Version (SUV)

19. akihesabu ya kuwa Mungu aweza kumfufua hata kutoka kuzimu; akampata tena toka huko kwa mfano.

20. Kwa imani Isaka akawabariki Yakobo na Esau, hata katika habari ya mambo yatakayokuwa baadaye.

21. Kwa imani Yakobo, alipokuwa katika kufa, akambariki kila mmoja wa wana wa Yusufu, akaabudu akiegemea kichwa cha fimbo yake.

22. Kwa imani Yusufu, alipokuwa amekaribia mwisho wake, alitaja habari za kutoka kwao wana wa Israeli, akaagiza kwa habari ya mifupa yake.

23. Kwa imani Musa, alipozaliwa, akafichwa miezi mitatu na wazazi wake, kwa sababu waliona kwamba ni mtoto mzuri; wala hawakuiogopa amri ya mfalme.

24. Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao;

25. akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo;

26. akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo.

27. Kwa imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana.

28. Kwa imani akaifanya Pasaka, na kule kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wao.

29. Kwa imani wakapita kati ya Bahari ya Shamu, kama katika nchi kavu; Wamisri walipojaribu kufanya vivyo wakatoswa.

30. Kwa imani kuta za Yeriko zikaanguka, zilipokwisha kuzungukwa siku saba.

31. Kwa imani Rahabu, yule kahaba, hakuangamia pamoja na hao walioasi; kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi kwa amani.

32. Nami niseme nini tena? Maana wakati usingenitosha kuleta habari za Gideoni na Baraka na Samsoni na Yeftha na Daudi na Samweli na za manabii;

33. ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba,

34. walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga. Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni.

35. Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora;

36. wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani;

37. walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya;

38. (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi.

39. Na watu hao wote wakiisha kushuhudiwa kwa sababu ya imani yao, hawakuipokea ahadi;

Kusoma sura kamili Ebr. 11