Agano la Kale

Agano Jipya

Zekaria 8:9-19 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Jipeni moyo! Sasa mnayasikia maneno ambayo mlitangaziwa na manabii wakati ulipowekwa msingi wa hekalu langu, kulijenga upya.

10. Kabla ya wakati huo, watu hawakupata mshahara kwa kazi zao wala kwa kukodisha mnyama. Hamkuwa na usalama kwa sababu ya adui zenu, maana nilisababisha uhasama kati ya watu wote.

11. Lakini sasa sitawatendea hao watu wa taifa hili waliosalia kama hapo zamani. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema.

12. Sasa nitaleta tena amani duniani, mvua itanyesha kama kawaida, ardhi itatoa mazao, na mizabibu itazaa kwa wingi. Nitawapa watu waliosalia wa taifa hili hayo yote yawe mali yao.

13. Enyi watu wa Yuda na watu wa Israeli! Wakati uliopita nyinyi mlionekana kuwa watu waliolaaniwa kati ya watu wa mataifa. Lakini sasa mimi nitawaokoeni, nanyi mtakuwa watu waliobarikiwa. Basi, msiogope tena, bali jipeni moyo!”

14. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Kama nilivyokusudia kuwatendea nyinyi maovu kwa sababu wazee wenu walinikasirisha, na wala sikuwaonea huruma,

15. vivyo hivyo nimekusudia kuutendea wema mji wa Yerusalemu na watu wa Yuda. Basi, msiogope.

16. Hivi ndivyo mnavyopaswa kufanya: Kila mmoja wenu na amwambie mwenzake ukweli. Mahakama yenu daima na yatoe hukumu za haki ziletazo amani.

17. Mtu yeyote miongoni mwenu asikusudie kutenda uovu dhidi ya mwenzake, wala msiape uongo, maana nayachukia sana matendo hayo. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

18. Neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi lilinijia mimi Zekaria:

19. “Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema hivi: Siku za mfungo za mwezi wa nne, mwezi wa tano, mwezi wa saba na mwezi wa kumi, zitakuwa nyakati za furaha na shangwe; zitakuwa sikukuu za sherehe kwa watu wa Yuda. Basi, pendeni ukweli na amani.”

Kusoma sura kamili Zekaria 8