Agano la Kale

Agano Jipya

Zekaria 12:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Neno la Mwenyezi-Mungu kuhusu Israeli. Mwenyezi-Mungu aliyezitandaza mbingu, aliyeiweka misingi ya dunia na kumpa mwanadamu uhai asema hivi:

2. “Nitaufanya mji wa Yerusalemu kuwa kama kikombe cha divai; na mataifa yaliyo kandokando yake yatakunywa na kuyumbayumba kama walevi. Mji wa Yerusalemu utakaposhambuliwa, hata miji yote ya Yuda itashambuliwa.

3. Siku hiyo nitaufanya mji wa Yerusalemu kuwa kama jiwe zito kwa watu wote: Yeyote atakayelinyanyua atajiumiza mwenyewe. Watu wa mataifa yote duniani wataushambulia mji huo.

4. Siku hiyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, nitamtia hofu kila farasi, na mpandafarasi wake nitamfanya kuwa mwendawazimu. Farasi wa mataifa mengine nitawapofusha. Lakini kabila la Yuda nitalilinda.

5. Ndipo viongozi wa Yuda watakapoambiana, ‘Wakazi wa Yerusalemu wamepata nguvu yao kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wao’.

6. “Siku hiyo, viongozi wa Yuda nitawafanya kama chungu cha moto mkali katika msitu; naam, kama mwenge uwakao kati ya miganda. Watayateketeza mataifa yote yaliyo kandokando yao. Lakini watu wa Yerusalemu wataendelea kuishi salama katika mji wao.

7. “Nami Mwenyezi-Mungu nitawasaidia kwanza jamaa za Yuda kusudi wazawa wa Daudi na wakazi wa Yerusalemu wasijione kuwa maarufu zaidi ya watu wengine wa kabila la Yuda.

8. Siku hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nitawalinda wakazi wa mji wa Yerusalemu; walio wanyonge zaidi miongoni mwao watakuwa na nguvu kama mfalme Daudi. Wazawa wa Daudi watashika usukani kuwaongoza watu wa Yuda kama malaika wangu mimi Mwenyezi-Mungu, naam, kama mimi Mungu mwenyewe.

Kusoma sura kamili Zekaria 12