Agano la Kale

Agano Jipya

Zaburi 18:20-37 Biblia Habari Njema (BHN)

20. Mwenyezi-Mungu alinipa tuzo kadiri ya uadilifu wangu;alinituza kwa vile mikono yangu haina hatia.

21. Maana nimefuata njia za Mwenyezi-Mungu,wala sikujitenga na Mungu wangu kwa uovu.

22. Nimeshika maagizo yake yote,sikuacha kufuata masharti yake.

23. Mbele yake sikuwa na hatia;nimejikinga nisiwe na hatia.

24. Mwenyezi-Mungu amenituza kadiri ya uadilifu wangu;yeye ajua kwamba mikono yangu haina hatia.

25. Wewe ni mwaminifu kwa walio waaminifu;mwema kwa wale walio wema.

26. Wewe ni mkamilifu kwa walio wakamilifu;lakini mkatili kwa watu walio waovu.

27. Wewe wawaokoa walio wanyenyekevu,lakini wenye majivuno huwaporomosha.

28. Wewe ee Mwenyezi-Mungu, waniangazia;walifukuza giza langu, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu.

29. Kwa msaada wako nakishambulia kikosi;wewe wanipa nguvu ya kuruka ukuta.

30. Huyu Mungu matendo yake hayana dosari!Ahadi ya Mwenyezi-Mungu ni ya kuaminika;yeye ni ngao kwa wote wanaomkimbilia usalama.

31. Nani aliye Mungu isipokuwa Mwenyezi-Mungu?Nani aliye mwamba wa usalama ila Mungu wetu?

32. Mungu ndiye anijaliaye nguvu kila upande;ndiye anayeifanya salama njia yangu.

33. Ameiimarisha miguu yangu kama ya paa,na kuniweka salama juu ya vilele.

34. Hunifunza kupigana vita,mikono yangu iweze kuvuta upinde wa shaba.

35. Umenipa ngao yako ya kuniokoa;mkono wako wa kulia umenitegemeza;wema wako umenifanikisha.

36. Umenirahisishia njia yangu;wala miguu yangu haikuteleza.

37. Niliwafuatia adui zangu na kuwakamata;sikurudi nyuma mpaka nimewaangamiza.

Kusoma sura kamili Zaburi 18