Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 9:9-25 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Wakamjibu, “Sisi, watumishi wako, tumetoka nchi ya mbali na tumekuja kwa maana tumesikia sifa za jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; tulipata habari za umaarufu wake na yote aliyoyafanya nchini Misri.

10. Tumesikia yote aliyowatenda wafalme wawili wa Waamori waliokuwa ngambo ya mto Yordani, mfalme Sihoni wa Heshboni na mfalme Ogu wa Bashani aliyekaa huko Ashtarothi.

11. Ndipo wazee wetu na wananchi wote wa nchi yetu, wakatuambia, tuchukue posho ya safari, tuje kukutana nanyi na kuwaambia kwamba sisi ni watumishi wenu; tafadhali fanyeni agano nasi.

12. Tazama mikate yetu ambayo ilikuwa bado moto tulipoichukua wakati tulipoondoka kwetu, lakini sasa imekauka na kuota ukungu.

13. Viriba hivi tulivijaza maji vikiwa vipya, lakini sasa vimepasukapasuka. Hata mavazi na viatu vyetu vimechakaa, kwani safari ilikuwa ndefu sana.”

14. Hivyo, Waisraeli wakachukua vyakula vyao, bila ya kumwuliza shauri Mwenyezi-Mungu.

15. Yoshua akafanya nao mkataba wa amani; akafanya agano kwamba atawaruhusu kuishi. Viongozi wa jumuiya ya Israeli wakawaapia kutekeleza mapatano hayo.

16. Siku tatu baada ya kufanya agano nao, Waisraeli wakagundua kwamba watu hao walikuwa jirani zao na waliishi miongoni mwao.

17. Basi, Waisraeli wakafunga safari, baada ya siku ya tatu wakafika katika miji yao. Miji hiyo ilikuwa Gibeoni, Kefira, Beerothi na Kiriath-yearimu.

18. Lakini Waisraeli hawakuwaua, maana viongozi wa jumuiya ya Israeli walikuwa wamewaapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Hivyo basi, jumuiya yote ikawanungunikia viongozi wao.

19. Lakini viongozi wa Waisraeli wakaiambia jumuiya ya watu wao, “Kwa vile tumewaapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, sasa hatuwezi kuwadhuru.

20. Tutawaacha waishi, ili tusije tukaadhibiwa kwa sababu ya kiapo tulichokula.

21. Waacheni waishi.” Hivyo Wagibeoni wakawa wanaitumikia jamii nzima ya Israeli, wakiwakatia kuni na kuwachotea maji, kama viongozi wa Waisraeli walivyosema.

22. Yoshua akawaita Wagibeoni na kuwauliza, “Kwa nini mlitudanganya kwamba mlitoka nchi ya mbali na hali nyinyi mnaishi miongoni mwetu?

23. Sasa, nyinyi mmelaaniwa na baadhi yenu daima mtakuwa watumwa wa kukata kuni na kuchota maji kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu.”

24. Wakamjibu Yoshua, “Tuliambiwa kwamba kwa hakika Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alimwamuru mtumishi wake Mose awaangamize wakazi wote wa nchi hii na kuwapa nyinyi nchi hii iwe mali yenu. Kwa hivyo, tulihofia maisha yetu na ndipo tukafanya jambo hili.

25. Sasa sisi tumo mikononi mwako, ututendee kama unavyoona inafaa.”

Kusoma sura kamili Yoshua 9