Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 9:17-27 Biblia Habari Njema (BHN)

17. Basi, Waisraeli wakafunga safari, baada ya siku ya tatu wakafika katika miji yao. Miji hiyo ilikuwa Gibeoni, Kefira, Beerothi na Kiriath-yearimu.

18. Lakini Waisraeli hawakuwaua, maana viongozi wa jumuiya ya Israeli walikuwa wamewaapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Hivyo basi, jumuiya yote ikawanungunikia viongozi wao.

19. Lakini viongozi wa Waisraeli wakaiambia jumuiya ya watu wao, “Kwa vile tumewaapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, sasa hatuwezi kuwadhuru.

20. Tutawaacha waishi, ili tusije tukaadhibiwa kwa sababu ya kiapo tulichokula.

21. Waacheni waishi.” Hivyo Wagibeoni wakawa wanaitumikia jamii nzima ya Israeli, wakiwakatia kuni na kuwachotea maji, kama viongozi wa Waisraeli walivyosema.

22. Yoshua akawaita Wagibeoni na kuwauliza, “Kwa nini mlitudanganya kwamba mlitoka nchi ya mbali na hali nyinyi mnaishi miongoni mwetu?

23. Sasa, nyinyi mmelaaniwa na baadhi yenu daima mtakuwa watumwa wa kukata kuni na kuchota maji kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu.”

24. Wakamjibu Yoshua, “Tuliambiwa kwamba kwa hakika Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alimwamuru mtumishi wake Mose awaangamize wakazi wote wa nchi hii na kuwapa nyinyi nchi hii iwe mali yenu. Kwa hivyo, tulihofia maisha yetu na ndipo tukafanya jambo hili.

25. Sasa sisi tumo mikononi mwako, ututendee kama unavyoona inafaa.”

26. Basi, alilowatendea ni kuwaokoa mikononi mwa Waisraeli ili wasiangamizwe; hivyo hawakuwaua.

27. Lakini kutoka siku hiyo, Yoshua aliwafanya hao kuwa wakata-kuni na wachota-maji kwa ajili ya jumuiya nzima ya Waisraeli na kwa ajili ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, popote pale Mwenyezi-Mungu alipochagua mpaka hivi leo.

Kusoma sura kamili Yoshua 9