Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 9:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Wafalme wote waliokuwa ngambo ya mto Yordani katika nchi ya milimani na kwenye tambarare na eneo lote la pwani ya bahari ya Mediteranea kuelekea Lebanoni, Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, waliposikia habari za Waisraeli,

2. wakakusanyika pamoja kwa nia moja ili kupigana vita na Yoshua na Waisraeli.

3. Lakini wakazi wa Gibeoni walipopata habari juu ya jinsi Yoshua alivyoitenda miji ya Yeriko na Ai,

4. waliamua kutumia hila. Wakatayarisha vyakula, wakapakiza magunia yaliyochakaa juu ya punda wao, viriba vilivyochakaa na kushonwa;

5. wakavaa viatu, nguo zilizochakaa na vyakula vyao vyote vilikuwa vikavu vilivyoota ukungu.

6. Basi, wakamwendea Yoshua kambini Gilgali, wakamwambia yeye na Waisraeli, “Sisi tumetoka nchi ya mbali; tafadhali tunaomba mfanye agano nasi.”

7. Lakini Waisraeli wakawajibu hao Wahivi, “Tunawezaje kufanya agano nanyi? Labda nyinyi mnaishi karibu nasi.”

8. Nao wakamwambia Yoshua, “Sisi tu watumishi wako.” Naye Yoshua akawauliza, “Nyinyi ni akina nani, na mnatoka wapi?”

9. Wakamjibu, “Sisi, watumishi wako, tumetoka nchi ya mbali na tumekuja kwa maana tumesikia sifa za jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; tulipata habari za umaarufu wake na yote aliyoyafanya nchini Misri.

10. Tumesikia yote aliyowatenda wafalme wawili wa Waamori waliokuwa ngambo ya mto Yordani, mfalme Sihoni wa Heshboni na mfalme Ogu wa Bashani aliyekaa huko Ashtarothi.

Kusoma sura kamili Yoshua 9