Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 8:9-21 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Basi, Yoshua akawaambia waende mahali pao pa kuvizia; nao wakajiweka magharibi ya mji wa Ai kati ya mji wa Ai na Betheli. Lakini Yoshua alilala usiku huo katika kambi ya Waisraeli.

10. Yoshua akaamka asubuhi na mapema, akawakusanya Waisraeli na kuelekea mjini Ai, akiwa pamoja na wazee.

11. Wanajeshi wote waliofuatana naye walikaribia mji na kupiga kambi kaskazini yake, ngambo ya bonde mkabala wa mji wa Ai.

12. Ndipo akachukua watu wengine 5,000 na kuwaweka wavizie kati ya mji wa Betheli na Ai, magharibi ya mji wa Ai.

13. Kikosi kikubwa kiliwekwa kaskazini mwa mji na wale waliobaki waliwekwa magharibi ya mji. Lakini usiku huo, Yoshua akalala bondeni.

14. Mfalme wa mji wa Ai alipoona hivyo, aliharakisha na kwenda kwenye mteremko wa kuelekea Araba ili akabiliane na Waisraeli vitani. Lakini hakujua kwamba mji wake ulikuwa umeviziwa kutoka nyuma.

15. Kisha Yoshua pamoja na watu wake wakajifanya kana kwamba wanashindwa, wakaanza kukimbia kuelekea jangwani.

16. Watu wote waliokuwa mjini waliitwa wawafuatie Waisraeli; na walipokuwa wanamfuatia Yoshua, walitoka na kwenda mbali na mji wao.

17. Hakuna mtu yeyote aliyebaki mjini Ai, waliuacha mji huo wazi wakaenda kuwafuatia Waisraeli.

18. Halafu Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Elekeza mkuki wako huko mjini Ai maana nitautia mji huo mikononi mwako.” Yoshua akaelekeza mkuki wake mjini Ai.

19. Mara Yoshua alipouelekeza mkuki wake kule Ai, kikosi kilichokuwa kikivizia upande mwingine kikatoka na kuingia mjini; kikauteka mji na kuuteketeza kwa moto.

20. Watu wa Ai walipotazama nyuma, wakaona moshi kutoka mjini ukipanda mpaka mbinguni. Nao hawakuwa na uwezo wa kukimbia upande wowote, maana Waisraeli waliwageukia hao waliokuwa wanawafuatia.

21. Yoshua na Waisraeli wote walipoona kuwa kikosi kilichokuwa kinavizia kimeuteka mji, na kwamba moshi ulikuwa unapanda juu, waliwageukia na kuanza kuwaua.

Kusoma sura kamili Yoshua 8