Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 8:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Usiogope, wala usiwe na wasiwasi wowote; wachukue wanajeshi wako wote uelekee mji wa Ai, kwani mfalme wa Ai nimemtia mikononi mwako, pamoja na watu wake, mji wake na nchi yake.

2. Mtautendea mji wa Ai pamoja na mfalme wake kama vile mlivyoutendea mji wa Yeriko pamoja na mfalme wake. Mali zake pamoja na mifugo yake mtakayoteka itakuwa ni mali yenu. Nendeni mwuvamie mji kutoka upande wa nyuma.”

3. Basi, Yoshua akaondoka, pamoja na wanajeshi wake wote kwenda Ai. Akawachagua watu hodari 30,000 na kuwaambia watangulie wakati wa usiku.

4. Akawaamuru hivi: “Nyinyi mtauvizia mji kutoka upande wa nyuma. Msiende mbali na mji, bali muwe tayari wakati wote.

5. Mimi, pamoja na watu wote walio pamoja nami, tutaukaribia mji. Watu watakapotoka nje kuja kutukabili kama hapo awali, sisi tutawakimbia.

6. Nao wataendelea kutufuatia mpaka wawe mbali na mji wao, maana watafikiri wametutimua kama walivyofanya hapo awali. Sisi tutawaacha watufukuze.

7. Hapo, nyinyi mtatokea kutoka huko mlikokuwa mnavizia na kuuteka mji, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atautia mji huo mikononi mwenu.

8. Mkishauteka mji mtauteketeza kwa moto, kama vile Mwenyezi-Mungu alivyoamuru. Hayo ndiyo maagizo mtakayofuata.”

9. Basi, Yoshua akawaambia waende mahali pao pa kuvizia; nao wakajiweka magharibi ya mji wa Ai kati ya mji wa Ai na Betheli. Lakini Yoshua alilala usiku huo katika kambi ya Waisraeli.

10. Yoshua akaamka asubuhi na mapema, akawakusanya Waisraeli na kuelekea mjini Ai, akiwa pamoja na wazee.

Kusoma sura kamili Yoshua 8