Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 3:10-17 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Yoshua akaendelea kusema, “Sasa mtajulishwa kabisa kwamba Mungu aliye hai yu miongoni mwenu na kwamba atawafukuza mbele yenu Wakanaani, Wahiti, Wahivi, Waperizi, Wagirgashi, Waamori na Wayebusi, bila kushindwa.

11. Tazameni, sanduku la agano la Bwana wa dunia yote, liko karibu kupita mbele yenu kuelekea mtoni Yordani.

12. Sasa, chagueni watu kumi na wawili kutoka makabila ya Israeli, kila kabila mtu mmoja.

13. Wakati nyayo za makuhani wanaobeba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, Bwana wa dunia yote, zitakapoingia katika maji ya mto Yordani, maji ya mto huo yataacha kutiririka. Na yale yatakayokuwa yanatiririka kutoka upande wa juu yatajikusanya pamoja kama rundo.”

14. Basi, watu waliondoka katika kambi zao ili kwenda kuvuka mto Yordani, nao makuhani wakiwa wamebeba sanduku la agano wanawatangulia watu.

15. Na mara tu hao waliobeba sanduku la agano walipofika Yordani na nyayo zao zilipokanyaga ukingoni mwa mto huo (mto Yordani hufurika wakati wa mavuno),

16. maji yaliyokuwa yanatiririka kutoka upande wa juu yalisimama na kurundikana mpaka huko Adamu kijiji kilicho karibu na mji wa Sarethani. Maji yaliyokuwa yanateremka kwenda bahari ya Araba, yaani Bahari ya Chumvi, yalitoweka kabisa, watu wakavuka mbele ya Yeriko.

17. Wakati Waisraeli walipokuwa wanavuka makuhani waliokuwa wanalibeba sanduku la agano walisimama mahali pakavu katikati ya mto Yordani mpaka taifa lote likavuka.

Kusoma sura kamili Yoshua 3