Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 3:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Asubuhi na mapema Yoshua pamoja na watu wote wa Israeli walianza safari kutoka Shitimu. Walipoufikia mto Yordani, walipiga kambi hapo kwa muda kabla ya kuvuka.

2. Baada ya siku tatu, viongozi walipita katikati ya kambi hiyo,

3. wakawaambia watu, “Mtakapoliona sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, limebebwa na makuhani Walawi, mtaondoka na kulifuata;

4. ndivyo mtakavyojua njia ya kupita maana hamjapita huku kamwe. Lakini msilikaribie mno sanduku la agano; muwe umbali wa kilomita moja hivi.”

5. Yoshua akawaambia watu, “Jitakaseni kwa kuwa kesho Mwenyezi-Mungu atatenda maajabu kati yenu.”

6. Kisha akawaambia makuhani, “Chukueni sanduku la agano, mtangulie nalo mbele ya watu.” Nao wakalichukua na kutangulia mbele ya watu.

7. Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua: “Leo hii, nitaanza kukutukuza mbele ya watu wote wa Israeli ili wajue kwamba, kama vile nilivyokuwa pamoja na Mose, ndivyo pia nitakavyokuwa pamoja nawe.

8. Utawaamuru hao makuhani wanaobeba sanduku la agano wasimame karibu na ukingo wa mto Yordani wakati watakapofika huko.”

9. Kisha Yoshua akawaambia Waisraeli: “Njoni karibu mpate kusikia maneno ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.”

10. Yoshua akaendelea kusema, “Sasa mtajulishwa kabisa kwamba Mungu aliye hai yu miongoni mwenu na kwamba atawafukuza mbele yenu Wakanaani, Wahiti, Wahivi, Waperizi, Wagirgashi, Waamori na Wayebusi, bila kushindwa.

Kusoma sura kamili Yoshua 3